Latest Posts

KUIBULIWA KWA ‘MADUDU’ KWENYE VITUO, NA WASIWASI KUHUSU UCHAGUZI WA HAKI SERIKALI ZA MITAA

Joto la uchaguzi wa serikali za mitaa nchini linaendelea kushika kasi kila baada ya siku, na hiyo inatokana na ukweli kwamba uchaguzi huo unatabiriwa kuleta ushindani mkubwa miongoni mwa vyama vya siasa nchini
Licha ya kwamba Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatambua uwepo wa vyama 19 hai lakini uhalisia uliopo ni kwamba huenda ‘vita’ ya uchaguzi huo inaweza kuhusisha vyama vitatu au vinne tu kwa ukubwa wake, ambapo vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF)
Kwa kusema hivyo haimaanishi tumebeza nafasi ya vyama vingine 15 la hasha, bali tunatambua uwepo wake ila mtazamo wa Watanzania walio wengi unaonekana kutoviamini na pengine havioneshi kuwa na uchu wa kuwa na ushindani kwenye uchaguzi huo
Hivi karibuni zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la mkazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa limefungwa rasmi nchini, na zoezi linaloendelea kwa sasa ni uhakiki wa majina na taarifa za waliojiandikisha katika uchaguzi huo, taarifa zinazopatikana kwenye mbao za matangazo zilizopo kwenye maeneo ya vilivyokuwa vituo vya kuandikisha, na kwenye ofisi za mamlaka mbalimbali za kiserikali
Hata hivyo kumekuwa na mjadala mkubwa unaoendelea sasa hapa nchini kuhusiana na uchaguzi huo, achana na ule unaolenga kuhoji endapo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Waziri mwenye dhamana ya ofisi hiyo kama ana anastahili kusimamia uchaguzi huo au la, nimesema hiyo si sehemu ya ninayolenga kueleza hapa kwa kuwa jambo hilo ni la kisheria na kwamba mjadala wake ni wa kisheria, ndio maana nami naungana na Watanzania wengine kusubiri kauli ya Mahakama kuhusiana na jambo hilo, lakini kwangu yeyote atakayesimamia kwangu  kawaida tu, kama TAMISEMI itaendelea kama inavyofanya sasa kwangu mimi sawa, kama Mahakama itasema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inapaswa kuchukua majukumu hayo kwangu mimi sawa, na hata kama Mahakama itaeleza jambo lingine kabisa yote nitayapokea, kutokana na ukweli kwamba masuala hayo ni ya kisheria
Mjadala ninaougusia hapa ni kutokana na zoezi hilo la kujiandikisha kwenye daftari la mkazi lililohitimishwa hivi karibuni, ambapo kabla, wakati na hata baada ya kufungwa kwa zoezi hilo  mjadala unashuhudiwa
Kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa haki, demokrasia na hususani vyama vya siasa vya upinzani nchini wakiibua madai ya uwepo wa matukio na viashiria vya udanganyifu vinavyotilia mashaka uchaguzi huo kuwa huru na haki
Kwa sasa (hasa kwenye mitandao ya kijamii) kumeshuhudiwa picha jongefu (video) na hata picha za kawaida ambazo bila shaka zimepigwa ‘kwa siri’ ambazo kwa kiasi kikubwa zinaonesha ‘madudu’ yanayoendelea kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura wakati na hata baada ya zoezi hilo kufungwa
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile lililoshuhudiwa kule mkoani Katavi lililokuwa limeibuliwa na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani humo Rhoda Kunchela na wenzake ambapo walituonyesha namna afisa muandikishaji alivyokuwa anatumia karatasi zisizokuwa rasmi kuandikisha wapiga kura, na alipoulizwa alidai kuwa daftari limejaa, mvutano wa eneo hilo tamati yake ilishuhudia vigogo hao wa CHADEMA Katavi wakikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo wakidaiwa kumfanyia fujo afisa mwandikishaji
Sambamba na hilo yapo madai kuwa kwenye baadhi ya maeneo watu walioandikishwa wameshafariki lakini majina yao yanasomeka kwenye mbao za matangazo kama ilivyoibuliwa kwenye kijiji kimoja’ huko mkoani Mbeya ambapo inaelezwa kwamba familia ya mtu huyo (aliyefariki lakini jina lake linadaiwa kuonekana kwenye mbao ya matangazo ya mmoja ya waliojiandikisha) imeshtushwa na hilo jambo ambalo limetengeneza maswali lukuki, kulikoni?
Yapo madai kwamba baadhi ya watu waliojiandikisha au kuandikishwa kwenye daftari la mkazi sio tu kwamba ni wanafunzi bali pia hawajakidhi vigezo stahiki vya kuandikishwa ikiwemo kukosa sifa ya umri stahiki unaohitajika
Zipo taarifa pia zinazodai kuwa baadhi ya maeneo watu wengine wameandikishwa kwenye kituo zaidi ya kimoja, haya na mengine mengi yamekuwa yakiibua maswali lukuki ya nini kilichopo nyuma ya pazia ya jambo hili, je ni bahati mbaya au mpango wa kupangwa?
Kama ni bahati mbaya unajiuliza inawezekanaje mtu anajiandikisha zaidi ya kituo kimoja halafu aseme ni bahati mbaya?, inawezekanaje afisa mwandikishaji aliyepata mafunzo aanze kuandikisha watu kwenye daftari lisilo rasmi halafu useme ni bahati mbaya?, inawezekanaje mwanafunzi ajipeleke kwenye kituo cha kuandikisha tena umri wake ukionekana haukidhi vigezo vya kuandikishwa halafu afisa mwandikishaji anampokea na anamjumuisha?, inawezekanaje?, inawezekanaje?, narudia kuuliza tena inawezekanaje?
Nikijiuliza maswali hayo napata ukakasi kuamini kwamba hayo yote yamekuja kwa bahati mbaya, na binafsi naamini sio dhambi kufikiri kuwa huenda yupo mtu au watu wanaoratibu njia mbaya kuelekea uchaguzi huo?, kama madai yanayozungumzwa yana uhalisia basi safari yetu ni ni nyembamba sana kufikia uwepo wa uchaguzi huru na wa haki, siko hapa kumnyooshea kidole mtu/ watu, au chama chochote cha siasa bali niko hapa kujiuliza kuwa kama haya yanayozungumzwa yana uhalisia nini maana yake?
Itakumbukwa kuwa haya yote yanachomoza wakati huu ambao serikali ya awamu ya sita (6) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayo mtihani mkubwa wa kuuaminisha umma wa wapenda haki na ukuaji wa demokrasia ndani na nje ya Tanzania kuwa sasa mambo yako safi, mara zote bila shaka serikali ikiongozwa na Rais mwenyewe ameeleza hayo kwa mapana yake hapa nchini na hata kwenye Jumuiya ya Kimataifa, sasa yale yalikuwa ni maneno bila shaka kila mmoja macho na masikio yake anayaelekeza sasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu (2024) na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani (2025) ili kujuwa yaliyomo yamoo?
Watu wengi iwe ndani au nje ya Tanzania wanajuwa kilichotokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wadau wa haki na ukuaji wa demokrasia hawatamani sio tu kuona bali kuota yale yaliyojiyokeza kwenye chaguzi hizo, sasa kama kuna ‘genge’ linalotaka kuturejesha huko sijuwi itakuwaje
Hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ambaye kiuhalisia ndiye msimamizi mkuu wa uchaguzi wa serikali za mitaa nchini amekanusha madai hayo, hususani madai ya wanafunzi kuuhishwa katika zoezi la uandikishaji, lakini kama hiyo haitoshi licha ya baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na nk, kutoa malalamiko na kasoro ya zoezi la mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini mapema leo, Jumanne Oktoba 22.2024 Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wake wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo Taifa CPA Amos Makala kimeeleza kuridhishwa na namna mambo yanavyoenda kuelekea uchaguzi huo
Jambo TV itaendelea kufuatilia zaidi ili kujuwa kinagaubaga undani wa madai hayo na uhalisia wa majawabu ya TAMISEMI.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!