Hitilafu ya umeme kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete imesababisha treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili (2) siku ya tarehe 30 Julai 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 31 Julai 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Jamila Mbarouk, hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama mfano wa ngedere au ndege mfano wa bundi wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system).
“Hitilafu ilisababisha umeme kukatika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) ambayo kitaalamu hujulikana kama (Instanteneous Overcurrent Protection Trip) majira ya saa 4:20 usiku” Imeeleza taarifa hiyo.
TRC imeeleza kuwa mafundi wake walifanikiwa kutatua changamoto na kurejesha umeme saa 6:30 usiku na treni kuendelea na safari kuelekea Dodoma, na kuwasili Dodoma majira ya saa 7:57 usiku.