Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa amesema bado kuna viongozi wa serikali na jamii ambao hawana utayari wa kufanya kazi na Watetezi wa haki za Binadamu.
Wakili Olengurumwa ameyasema hayo na kuongeza licha ya uwepo wa viongozi hasa katika ngazi za juu kuwa na utayari wa kufanya kazi na Watetezi hao lakini bado kumekuwa na baadhi ya viongozi katika ngazi za chini wakiwemo baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa ambao wamekuwa hawana utayari.
Ametoa kauli hiyo akizungumza na waandishi wa Habari jijini Mwanza katika mafunzo juu ya ufuatiliaji,utunzaji ,utoaji wa taarifa sambamba na namna ya kukabiliana na hatari wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku Watetezi hao.
“Changamoto ni nyingi ukiacha za kisheria na nyingine za kiutendaji kuna viongozi wengine bado hawaelewi umuhimu wa kufanya kazi na Watetezi wa Haki za Binadamu,kuna viongozi wengine bado hawataki kufanya kazi na Watetezi wa haki za Binadamu” amesema Olengurumwa
Mbali na hivyo amesema wao kama Mtandao furaha yao ni kuona Watetezi hao wanafanya kazi katika mazingira huru huku akisisitiza kuwa kazi namba moja ya Mtandao ni kuwatetea Watetezi hao.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu ( 23- 26 July 2024) jijini Mwanza kwa ajili ya kujenga uelewa kwa mashirika wanachama yanayotetea Haki za Binadamu kanda ya ziwa na waratibu wake wa kanda juu ya ufuatiliaji,utunzaji ,utoaji wa taarifa sambamba na namna ya kukabiliana na hatari wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku Watetezi hao.