Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupanda zaidi ya miti 100 katika Kituo cha Mafunzo ya Waraibu wa Dawa za Kulevya (Sober House) jijini Mbeya.
Zoezi hilo lililohusisha upandaji wa miti ya matunda na vivuli, limelenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika utunzaji wa mazingira, huku likiwa na faida ya moja kwa moja kwa waraibu wanaopata mafunzo kituoni hapo.
Kamishna Msaidizi wa DCEA, Zulpha Chenga, amesema kuwa miti hiyo itasaidia kutengeneza mazingira rafiki ya kupumzikia na kupata matunda kwa vijana walio katika hatua za kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine, Ofisa wa Mamlaka hiyo, Adrick Ndelwa, ametoa onyo kali kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha dawa za kulevya (kama bangi na mirungi), akiwataka kuacha mara moja na badala yake wajikite katika mazao halali. Amebainisha kuwa mapambano hayo yanaendelea kuzaa matunda kwani waraibu wengi wameshamaliza matibabu na sasa wamerudi katika jamii kulijenga taifa.

Maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais Samia (Januari 27) nchi nzima yameambatana na kampeni mbalimbali za kijani, zikisisitiza kauli mbiu ya utunzaji wa mazingira kama kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita.
