Hivi karibuni kumeshuhudiwa ukakasi wa maamuzi unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini hasa katika suala la usimamizi wa sheria zinazohusu vyama vya siasa na wanasiasa wenyewe
Malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani nchini ambayo yamesikika kwa ukubwa wake siku za karibuni, ni yale yanayodai kuwa Jeshi hilo limekuwa likileta mkakanganyiko wa maamuzi kwa vyama vya siasa kwani yale ambayo yanakatazwa kufanywa na vyama vya upinzani yanabarikiwa kufanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) anbachoni chama dola nchini
Iko mifano mingi inayochochea hoja hiyo kukubalika na wengi, lakini miongoni mwake ni pale ambapo Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) lilipoandaa maadhimisho ya siku ya vijana Duniani yaliyopangwa kufanyika mkoani Mbeya yaliota mbawa baada ya maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo CP Awadh Juma Haji kuendesha oparesheni kali iliyoambatana na vipigo na udhalilishaji kwa viongozi waandamizi wa chama hicho ili tu kuzuia shughuli hiyo, jambo ambalo kwao lilifanikiwa
Hata hivyo, mkanganyiko wa jambo hilo umejitokeza pale tu ilipokumbukwa kuwa siku chache zilizopita Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) waliratibu shughuli kama hiyo na ikafanikiwa kwa mafanikio makubwa, ambapo maelfu ya vijana na wanachama wa chama hicho tawala walikutana kwenye uwanja wa New Amani Complex, Zanzibar huku Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo,
Kitendo cha UVCCM kufanikisha jambo lao huku wakipewa ushirikiano wa kina kutoka kwa Jeshi la Polisi, huku upande wa BAVICHA wakiambulia vipigo, kuwekwa korokoroni na manyanyaso ya kila aina aina inatoa taswira kuwa Jeshi la Polisi Lina kasumba ya upendeleo
Mfano mwingine ninaoweza kuutoa hapa ni pale ambapo unaona baadhi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CCM wanapotoa lugha za kuudhi, matusi, kejeli, udhalilishaji na hata pengine kutoa kauli zinazotishia uhai wa wengine lakini Jeshi la Polisi liko kimya na halichukui hatua yoyote, lakini hoja kama hizo ikiwa kinyume chake tu wapinzani wanaona ‘chamtemakuni’, hilo ndilo Jeshi la Polisi linalonyooshewa kidole kwa kufanya maamuzi yanayotengeneza maswali lukuki kwa jamii
Iko mifano mingi sana kuhusu weledi wa Jeshi la Polisi na namna linavyoshughulikia masuala ya wanasiasa wa upinzani na vyama vyao, kwa njia ya ‘mkono wa chuma’
Kiini cha makala hii fupi kinakuja kufuatia kuiona barua iliyoandikwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mpanda kwenda kwa CHADEMA Mpanda, barua ambayo inaonyesha wazi kuwa Jeshi hilo limezuia mikutano ya hadhara ya chama hicho iliyotarajiwa kufanyika Mpanda kwa ajili ya kutoa hamasa kwa jamii kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa
Katika barua hiyo yenye Kumb No. CGB.497/504/10 iliyotolewa Oktoba 08.2024 iliyosainiwa na Mahemba E. Kavalambi ambaye ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Mpanda, na nakala zake kupelekwa kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Mkuu wa wilaya ya Mpanda na DSO wa Mpanda kwa taarifa, imebainisha kuwa kutokana na muongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kuwapata viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27.2024 na tangazo la uchaguzi la lililotolewa Agosti 15.2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ambayo inavielekeza vyama vyote vya siasa nchini kwa kutokufanya mikutano ya hadhara tangu tarehe ya tangazo husika lilipotolewa na badala yake vyama hivyo viendelee kufanya vikao vya ndani ili kuimarisha vyama vyao
Aidha, barua hiyo imeendelea kufafanua kuwa tangazo hilo limetoa nafasi kwa taasisi binafsi kuendelea kutoa elimu ya mpiga kura, na kwamba hamasa inayohusiana na uchaguzi huo itatolewa na msimamizi wa uchaguzi
Barua hiyo ya Jeshi la Polisi Mpanda iliyokuwa inajibu barua ya CHADEMA Mpanda ya Oktoba 04.2024 yenye Kumb No.UCHG.SZM/W/MPN/VOL.01/2024 imeendelea kuikumbusha CHADEMA Mpanda kurejea kukumbuka kikao cha Septemba 29.2024 kilichoitishwa na Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Mpanda ambaye inatajwa kuwa aliwaita wadau wote wa uchaguzi wa pamoja na viongozi wote wa vyama vya siasa Mpanda ambapo aliwasomea maelekezo na ratiba nzima ya uchaguzi huo, hivyo Jeshi la Polisi Mpanda likaishauri CHADEMA Mpanda kutekeleza maelekezo ya tangazo hilo la uchaguzi, sambana na kurejea barua nyingine ya Jeshi la Polisi Mpanda iliyotumwa kwa CHADEMA Mpanda Oktoba 06.2024 ikiwa na Kumb. No. CGB.497/504/09
Ukiisoma barua ile unaona wazi kabisa kwamba Jeshi la Polisi limesimamia msingi ya kisheria, kikanuni na miongozo kadhaa kama ilivyorejewa, hapo sina tatizo na napongeza sana, lakini ukiisoma barua ile kwa undani na kuichambua utagundua kuwa sababu iliyopelekea CHADEMA kule Mpanda kupigwa marufuku mikutano yao si la Mpanda pekee bali ni ya Kitaifa kwa hiyo kwa muktadha huo sababu kama hiyo tubataraji itolewe kwa vyama vyote na wanasiasa wote hapa nchini kwa sasa, bila kujali hiki ni chama ‘Y’ au ‘X’ ikizingatiwa kuwa kwa sasa wote wako mawindoni kuelekea chaguzi zilizopo mbele yetu kama Taifa hususani uchaguzi wa serikali za mitaa
Lakini kilichonifanya niandae makala hii ni pale ninaposhuhudia viongozi waandamizi wa CCM wanaendelea kufanya mikutano hiyo na kwa kiasi kikubwa kama sio zote ni sehemu ya maandalizi ya chaguzi hizo, maana majukwaa yao kwa kiasi kikubwa yanatumika kutoa hamasa ya chaguzi hizo
Mfano wa wazi kabisa ni wa Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye kwa sasa anaendelea na ziara zake huko Kanda ya Ziwa, akianzia mikoa ya Simiyu, Shinyanga nk
Katika kila sehemu anayopita yeye na msafara wake anapewa ushirikiano mkubwa sana usioelezeka na Jeshi la Polisi na viongozi waandamizi wa serikali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa mikoa, Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi nk
Sasa swali langu kwa Jeshi la Polisi, kwa nini CHADEMA muikataze kufanya mikutano wakati huohuo CCM mnaipa baraka zote?, hamuoni kufanya hivyo ni sawasawa na kutuonyesha kuwa ninyi mmekuwa mkiibeba na kuisaidia CCM na kuwakandamiza wapinzani wa CCM?
Kwa hili natamani sana kuona serikali, CCM na hasa Jeshi la Polisi nchini kujitafakari kwenye mwenendo wake.