Latest Posts

LADIES CONNECT 2025: WANAWAKE WAASWA KUJITOKEZA NA KUPAMBANIA NDOTO ZAO

Kongamano la Ladies Connect 2025 limefanyika Machi 29, 2025, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), likiwaunganisha wanawake zaidi ya 200 kwa lengo la kufungua fursa na kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali.

Tukio hilo limeandaliwa na Serikali ya Wanafunzi wa UDSM (DARUSO) chini ya Makamu wa Rais wake, Neeral Paresh Solank, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Balozi Liberata Mulamula.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Balozi Mulamula amewataka wanawake, hususan wanafunzi wa chuo hicho, kuongeza jitihada katika kufanikisha ndoto zao.

“Nimejumuika hapa na wanafunzi wa chuo hiki, hususani wanawake, ambapo tumepata nafasi ya kujadili mambo kadhaa. Katika siku hii ya Mwanamke wa Shoka, tumewahimiza waongeze jitihada zaidi katika kupambania ndoto zao,” amesema.

Aidha, ameeleza kufurahishwa na uongozi wa wanawake ndani ya DARUSO, akisema hatua hiyo inaonesha kuwa wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi na kufanya mabadiliko.

“Nimefurahishwa kuona Makamu wa Rais wa DARUSO ni mwanamke. Tumezoea kuona wanaume wakiongoza serikali nyingi za wanafunzi, lakini hapa ni tofauti. Hii inaonesha kuwa wanawake wakiamua, wanaweza,” ameongeza.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa DARUSO, Neeral Paresh Solank, ameeleza kuwa kongamano hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwapatia wanafunzi maarifa na fursa mpya.

“Tumejifunza kuhusu mada mbalimbali na kupata fursa tofauti kupitia kongamano hili. Naamini wanafunzi wenzangu wataenda kulitumia vyema na kuyafanyia kazi mafunzo tuliyoyapata,” amesema Solank.

Kongamano la Ladies Connect 2025 limeonesha jinsi wanawake wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika uongozi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ujumbe mkubwa kutoka kwa viongozi wa kongamano hilo ni kwamba wanawake wanapaswa kujitokeza, kujifunza, na kutumia fursa zilizopo kufanikisha malengo yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!