Latest Posts

LHRC YASISITIZA SERIKALI KURIDHIA MKATABA WA KIMATAIFA KUPAMBANA NA UTEKAJI NA KUTOWEKA

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo kimeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahanga wa Matukio ya Kutoweka na Utekaji kwa kutoa wito kwa serikali ya Tanzania kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi kwa Watu Wote dhidi ya Kupotea na Kutekwa wa mwaka 1994.

Katika taarifa yake iliyotolewa Dar es Salaam, Agosti 30, 2024, LHRC imeungana na wadau wa haki za binadamu duniani kote kuwakumbuka wahanga wa matukio haya ya kikatili, huku ikielezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matukio ya utekaji na kutoweka nchini Tanzania. Kituo hicho kimesema matukio haya yamezidi kuwaathiri familia na jamii, na kuleta taharuki katika maeneo mbalimbali.

“Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko la matukio ya watu kutoweka na kutekwa katika mazingira tatanishi. Hii ni hali inayozidisha hofu na ukosefu wa amani katika jamii zetu,” alisema Dkt. Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC.

Katika taarifa hiyo, LHRC imeeleza kuwa mkataba huo wa kimataifa unatoa mfumo madhubuti wa kushughulikia matukio ya utekaji na kutoweka, na kwamba kuridhia mkataba huo kutasaidia kuweka ulinzi thabiti kwa wananchi wa Tanzania.

“Kuridhia mkataba huu siyo tu kutaiwezesha Tanzania kudhibiti vitendo vya utekaji, bali pia itaongeza imani ya wananchi juu ya ulinzi na usalama wao,” aliongeza Dkt. Henga.

LHRC pia imeitaka serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama katika ngazi za jamii kwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti matukio haya, na kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya malalamiko ya matukio ya hivi karibuni, hasa yale yanayoathiri watoto, wanawake, na jamii kwa ujumla.

LHRC imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha ulinzi wa haki za binadamu na kuhakikisha kuwa wahanga wa matukio haya wanapata haki ikiwamo fidia, huduma za matibabu, na usaidizi wa kisaikolojia kwa wahanga na familia zao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!