Watanzania wametakiwa kutumia haki zao za kikatiba kupiga kura katika uchaguzi utakaofanyika nchini baada ya kukamilisha zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kama ilivyoelezwa katika ibara ya 5(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Wito huo umetolewa siku ya Jumatatu Julai 22, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dkt. Anna Henga alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwamba Watanzania wote wenye sifa zilizoainishwa kikatiba wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi.
“Mtu atakuwa na sifa za kuandikishwa iwapo ni raia wa Tanzania, ametimiza umri wa miaka kumi na nane, hajaondolewa sifa za kuandikishwa na sheria nyingine, atatimiza umri wa miaka kumi na nane kabla au ifikapo siku ya uchaguzi, ni mkazi wa kawaida katika jimbo au kata ambayo anaomba kuandikishwa, ana akili timamu, hajatiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifo au hatumikii kifungo kwa kosa ambalo adhabu yake imezidi miezi sita, hajawekwa kizuizini kwa amri ya Rais na hana utii wa nchi nyingine tofauti na Tanzania” Ameeleza Dkt. Henga.
Aidha Dkt. Henga amesema kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kufanya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura angalau mara mbili ndani ya miaka mitano, hivyo LHRC kama taasisi iliyopewa ithibati na Tume hiyo ya kutoa elimu ya mpiga kura katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura imewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika vituo vya uandikishaji vilivyotolewa na Tume kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 mpaka pale zoezi litakapokuwa limefikia tamati.
Vilevile amesema zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao kwa sasa wana umri wa miaka kumi na nane au wale ambao watatimiza umri huo pale itakapofika mwaka 2025, wapiga kura ambao wakati Tume inafanya zoezi la uboreshaji wa daftari mwaka 2018/2019 hawakupata fursa hiyo.
“Aidha litatoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao, mathalani kwa mfano, mtu amekuwa padri, sheikh, mchungaji, daktari au kipindi anaandikishwa alikuwa hajaolewa na sasa ameolewa au jina lake limekosewa na anataka kurekebisha” Ameeleza Dkt. Henga.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litazinduliwa tarehe 20 Julai 2024 mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, ambapo wakati huohuo zoezi hilo litafanyika katika mikoa ya Katavi na Tabora kuanzia tarehe 20 mpaka 26 ya mwezi Julai mtawalia.
Baada ya mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, zoezi hilo litafuatiwa na mikoa ya Geita na Kagera, Mwanza na Shinyanga, Simiyu, Singida na baadhi ya wilaya za mkoa wa Manyara huku zoezi zima likitarajiwa kukamilika tarehe 5 ya Mwezi Machi ya mwaka 2025.