Kwanza wakati naanza Makala hii kama hufahamu naomba nikujuze tu kuwa Hezbollah ni chama tu cha kisiasa na chenye jeshi na utawala wake, kilichopo nchini Lebanon kikiwa kinawakilisha bungeni kwa sasa ni chama cha nne chenye wawakilishi wengi bungeni. Pia vyama vyenye wawakilishi wengi kinaanza chama cha Lebanese force 19, Free Patriotic movement 16, na amal movement 14.
Sasa Hezbollah (“Chama cha Mwenyezi Mungu”) ni chama cha kisiasa na kijeshi cha Kiislamu wa dhehebu la Kishia lenye makao yake nchini Lebanon. Ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 wakati wa Vita vya Kiraia vya Lebanon, awali kama mwitikio wa uvamizi wa Israel nchini Lebanon mwaka 1982. Kwa muda, limekua na kuwa nguvu kubwa ya kisiasa, kijeshi, na kijamii nchini Lebanon na Mashariki ya Kati kwa ujumla.
Kuanzishwa kwa Hezbollah
Hezbollah ilianzishwa mwaka 1982 na kundi la maulamaa wa Kishia, wengi wao wakiwa wamevutiwa na Mapinduzi ya Iran ya 1979 na kuathiriwa na uongozi wa kidini wa Iran, hasa Ayatollah Khomeini. Malengo yake ya awali yalijumuisha kupinga uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon, kukuza maslahi ya kisiasa na kijamii ya Waislamu wa Kishia, na kuanzisha dola ya Kiislamu nchini Lebanon, ingawa lengo hili limebadilika kwa muda.
Wakati wa Vita vya Kiraia vya Lebanon (1975-1990), Hezbollah ilikua nguvu kubwa, ikipata uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya Kishia ya Lebanon, ambayo ilihisi kutengwa kisiasa. Iliungwa mkono na Iran na Syria kwa mafunzo ya kijeshi, silaha, na msaada wa kifedha. Wakati huo kikiongozwa na Abbas al-Musawi ambaye aliuawa mwaka 1992 yeye aliongoza kwa miezi 9 tu na kumuachia nafasi Hassan Nasrallah
Uvamizi wa Israel na Kusini (1980s-2000)
Lengo kuu la Hezbollah katika miaka ya 1980 na 1990 lilikuwa kupinga uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon. Israel ilikuwa imeanzisha eneo la usalama kusini mwa Lebanon, ambapo iliunga mkono jeshi la eneo hilo (SLA). Hezbollah ilianzisha vita vya msituni na mashambulizi ya kujitoa mhanga dhidi ya vikosi vya Israel na nafasi za SLA. Pia ilihusika na utekaji nyara na milipuko kadhaa wakati huu, ikiwemo mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani na Ufaransa huko Beirut mwaka 1983, ambayo yaliua mamia ya walinda amani.
Mwaka 2000: Kuondoka kwa Israel pikutoka Lebanon
Mwaaka 2000, baada ya miaka ya mapigano, Israel iliondoa vikosi vyake kutoka kusini mwa Lebanon, tukio lililotazamwa kwa kiasi kikubwa kama ushindi mkubwa kwa Hezbollah. Tukio hili liliinua umaarufu wa Hezbollah nchini Lebanon, hasa kati ya jamii ya Kishia, na kuwa hatua muhimu katika jukumu la kundi hilo katika siasa za Lebanon na eneo lote.
Hezbollah kama Chama cha Kisiasa (1990s hadi sasa)
Hezbollah Iliingia rasmi katika siasa za Lebanon mwaka 1992, ikishinda viti 12 kati ya 128, mwaka 1996 ikashinda viti 7 na 2000 ikashinda viti 10 ambapo kwa sasa bungeni kwa sasa wana viti 13 kati ya 128 huku ikiungwa na vyama vingine kama THE FREE PATRIOTIC MOVEMENT (FPM) – 18 SEATS ikiwa ni chama kikubwa zaidi cha kikristo chanye nguvu bungeni na kinachomuunga Hezbollah, katika Bunge la Lebanon. Kwa muda, Hezbollah imekuwa muhimu katika siasa za Lebanon, ikishirikiana na vyama vingine na kuwa sehemu ya serikali.
Hezbollah pia inatoa huduma kubwa za kijamii, zikiwemo shule, hospitali, na misaada, ambazo zimeongeza uungwaji mkono wake miongoni mwa jamii ya Kishia ya Lebanon.
Vita vya Lebanon vya 2006
Mwaka 2006 vilianza vita katika taifa la Lebanon ambavyo vilivyoanza baada ya Hezbollah kufanya shambulio la kuvuka mpaka na kuwateka nyara wanajeshi wawili wa Israel. Hii ilisababisha vita vya siku 34 kati ya Hezbollah na jeshi la Israel, ambavyo vilisababisha vifo vingi na uharibifu wa mali nchini humo. Licha ya uharibifu huo, Hezbollah iliibuka na nguvu zake za kijeshi kwa kiasi kikubwa zikiwa hazijapunguzwa, na kiongozi wake, Hassan Nasrallah, alidai “ushindi wa kiungu” dhidi ya Israel, na hivyo kuongeza umaarufu wa kundi hilo katika ulimwengu wa Kiarabu.
Mingoni mwa makundi ya kiislam na kijeshi yaliyohusika katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria kuanza mwaka 2011 ni Hezbollah ambapo ilihusika katika kuuunga mkono utawala wa Bashar Al Assad, ikituma wapiganaji kusaidia vikosi vya serikali ya Syria. Hii ilionyesha mabadiliko ya jukumu la Hezbollah kutoka kundi la upinzani linalozingatia Lebanon pekee na kukifanya kazi katika muktadha mpana wa Mashariki ya Kati.
Tuongelee vita vikubwa na mashambulizi ya viongozi wa Hezbollah kwa Mwaka huu
Huenda huu ukawa miongoni mwa miaka michungu zaidi kwa makundi haya yanayopigana na nchi ya Israel ikiwemio kundi la Hamas ambapo kwa mwaka huu pia kiongozi wao Mkuu wa Kisiasa Ismail Hanniyeh aliuawa na Israel katika nchi ya Iran tarehe 31 mwezi wa saba mwaka huu. Kisha tarehe 27 mwezi wa 9 akauawa Nasrallah wa Hezbollah
Kuendelea kwa teknolojia kumekuwa kama mwiba kwa kundi hili la Hezbollah mfano kuuawa kwa Fuad Shukr ni kwa sababu ya teknolojia tena ilikuwa hivi mwezi wa January, kuna kamanda mwingine wa ngazi za juu wa Hezbollah alikuwa alifuatiliwa kwa usongo mkubwa na Mossad.
Huyu anaitwa Fuad Shukr. Huyu ni moja ya waanzilishi wa mwanzo kabisa wa tawi la kijeshi la chama cha Hezbollah (Jihad Council) na swahiba wa karibu wa viongozi wa juu wa Hezbollah.
Baada ya kumfuatila kwa wiki kadhaa hatimaye wakapata uhakika wa kumshambulia.
Siku ambayo wanamshambulia walitumia mbinu rahisi mno lakini ilizaa matunda. Nje kabisa ya jiji la Beirut kuna kijiji kinaitwa Beit Yahoun ambacho Mossad walikuwa wanafahamu Faud hupendelea kwenda kwa ajili ya kusalimu familia yake ambayo inaishi hapo.
Siku hii walikuwa wanataka uhakika waweze kujua kama yupo hapo kijijini. Moja ya jasusi wa kike wa Mossad akampigia simu binti wa Faud akijifanya ni mtumishi wa chuo kikuu cha AUB (American University of Beirut) ambacho binti huyo alikuwa anasoma.
Akamweleza binti huyu kuhusu fursa ya kusafiri kwenda ufaransa kwa wiki mbili kwa ajili ya masomo ya vitendo, fursa ambayo imetokea ghafla na mwalimu wake (akamtaja na jina) amempendekeza yeye binti kuwa moja wapo ya wanafunzi wa kusafiri. Hivyo akamtaka binti ampe uhakika kama anaweza kusafiri kwa ghafla hivyo ama kama hawezi nafasi hiyo awekwe mwanafunzi mwingine.
Binti akajibu kwamba anahitaji ruhusa ya wazazi ndipo atoe uhakika kama atakwenda ama la. Binti akaelezwa muda wa kazi wa siku hiyo usiishe kabla hajarejesha majibu kwenye ofisi husika chuoni kama yuko ‘interested’ ama la. Binti akajibu kwamba atatoa majibu dakika hiyo hiyo anawauliza wazazi wake kwani wapo nyumbani.
Na hicho ndicho Mossad walikuwa wanakitaka. Uhakika wa uwepo wa baba yake hapo nyumbani
Muda mchache baadae bomu la PGM likapiga nyumba na kumuua Faud mwenyewe, binti yake, mkewe, mtoto wake wa kiume anaitwa Abbas Raad, pamoja na wapiganaji watano wa Hezbollah ambao walikuwa pamoja naye hapo kwake.
Mfululizo wa mashambulizi haya mahususi, na ya hakika yalifanya Hezbollah ifanye tathimini ya kina kujua ni namna gani ambayo Mossad wanapata intelijensia nzuri kiasi hiki mfululizo.
Baada ya wiki kadhaa za uchunguzi, kitengo cha counter-intelligence cha Hezbollah kinachojulikana kama “Amn Al-Muddad” wakaja na majibu. Kwamba, mawasiliano yao ya simu na vifaa vya kieletroniki ya organisation nzima yako ‘compromised’ kwa sehemu kubwa. Na ndipo wakabaini kwamba karibia mashambulizi yote hayo mfululizo yaliyofanywa na Israel dhidi yao kwa mwezi January, yalifanikiwa kutokana na Mossad kudukua simu zao za mikononi ama vifaa vya kompyuta. Kiongozi mkuu Hassan Nasrallah tarehe 13 February mwaka huu 2024. Alitoa onyo kwamba, simu za mikononi ndani ya Lebanon kwa sasa zimekuwa hatari zaidi hata ya mashushushu wa mossad.
Na ndipo hapa uongozi wa juu wa Hezbollah wakafikia uamuzi wa kupiga marufuku viongozi, wanachama na wapiganaji wao kutumia simu za mkononi, simu za mezani, vifaa vya kompyuta na teknolojia yeyote ya kisasa.
Badala yake mawasiliano yote muhimu yafanyike kwa njia ya mdomo kupitia kwa vijumbe/mesenja.. Sa’in. Na maagizo yafikishwe kwa kuonana ana kwa ana.
Na wanachama na wapiganaji wao wote waachane na simu za mkononi na badala yake warejee kwenye enzi za kale za kutumia pagers kwa ajili ya mawasiliano ya dharura na maagizo yenye kuhitaji uharaka wa utekelezaji.
Kuuawa kwa kiongozi mkuu Hassan Nasrallah
Inasemekana kwamb shushushu aliyeiambia Israel kuwa Nasrallah alikuwa njiani kuelekea kwenye bunker alikuwa Muirani. Huenda taarifa hizi zimetolewa maalum kijasusi ili kuwatengenezea ugomvi Hezbollah na mshirika wake ambaye ni Iran
Ripoti za mpango wa shambulio zinaonyesha kuwa Israel ilikuwa ikifuatilia eneo hilo kwa muda. Kamanda wa Kikosi cha 69 cha ndege za F-15I kilichofanya shambulio, ambaye alitajwa katika vyombo vya habari vya Israeli kama Lt.Col M, alisema wahudumu wa ndege walikuwa wakijiandaa kwa “siku kadhaa,” ingawa walijulishwa kuhusu lengo lililokusudiwa masaa machache tu kabla. Ndege za F-15I zilikuwa zimeandaliwa kushambulia na kuharibu chini ya ardhi, zikiwa na kiasi kikubwa cha milipuko, ambacho pia kilikuwa na uwezo wa kuondoa majengo yaliyo juu.
Video iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel Jumamosi ya ndege “zinazoondoka kwa shambulio kutoka kwenye uwanja wa ndege wa Hatzerim” ilionyesha F-15I nane zilizotengenezwa Marekani. Ndege moja inayondoka ilikuwa imejaa makombora kadhaa, chini ya mabawa na nyuma. Wataalamu walisema zilionekana kuwa mabomu ya BLU-109 ya pauni karibia kilo 900, ya daraja ambalo marekani iliwahi kukikataza Israel kutoyatumia hasda katia ukanda wa Gaza kwenye maeneo yenye watu wengi.
Justin Bronk, mtaalamu wa anga kutoka taasisi ya Royal United Services Institute (Rusi), alisema kuwa jeshi la anga la Israeli labda lingetumia makombora ya 2,000lb ya pamoja ya mashambulizi ya moja kwa moja yaliyopangwa na fuses zinazotakiwa kulipuka baada ya jengo au ardhi kugongwa. Maafisa wa jeshi la anga la Israeli walisema kwamba wakati wa shambulio, lililojulikana kama Operesheni Mpango Mpya, karibu silaha 100 zilitumika na mabomu yalitupwa “kila sekunde mbili.”
Majengo manne ya makazi yalipigwa, matatu yakiwa yameharibiwa kabisa, na kuacha tu mashimo yanayowaka, na mengine mawili yalidhurika katika shambulio hilo. Makadirio ya awali kwenye eneo hilo yalionyesha kuwa watu 300 wanaweza kuwa wameuawa, ingawa hesabu rasmi ya Lebanon ilikuwa ni watu 11 waliouawa na 108 kujeruhiwa. Israel ilisema kwamba ilikuwa imeua zaidi ya wanachama 20 wa Hezbollah na kwamba shambulio lilikuwa halali kwa sababu “Nasrallah kwa makusudi alijenga makao makuu ya Hezbollah chini ya majengo ya makazi katika Dahiya.”
Brig Gen Amichai Levine, kamanda wa uwanja wa ndege wa Hatzerim ambapo Kikosi cha 69 kimepangwa, alitoa maelezo zaidi kuhusu mipango hiyo. Changamoto ya kwanza, katika kile alichokiita kwa baridi “operesheni za kuondoa,” ilikuwa ni taarifa sahihi; ya pili, alisema katika mkutano wa waandishi wa habari, ilikuwa kuhakikisha kuwa lengo “halikimbii wakati ndege ziko njiani au silaha ziko njiani kuelekea kwenye lengo” – kwa mfano, kwa kutopokea onyo la mapema kwamba ndege za kivita ziko angani na njiani.
Ndipo shambulizi likafanyika lakini taarifa ya kuuawa kwa Hassan Nasrallah ahikutoka papo hapo ilitoka baada ya muda kidogo ikimaanisha kuwa Israel walitaka kuthibitisha hili juu ya kifo ndipo watangaze. Na hawa ndio Hezbollah kwa uchache wake.