Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amezindua Ligi ya ‘Piga Kura Piga Mpira Jiandikishe’ kwenye kijiji cha Nangumi kata ya Mayanga mkoani Mtwara.
Ligi hiyo iliyozinduliwa Juni 30, 2024 lengo lake ni kuhamasisha kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura na kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa 2024 iliyoandaliwa na Diwani wa kata ya Mayanga Arif Suleiman Premji.
DC Mwanahamisi Munkunda amempongeza diwani huyo kwa kuandaa ligi hiyo na ameelekeza ligi hiyo kuwa ligi ya wilaya nzima ili kuzidi kuhamasisha wananchi hususani vijana kwenda kujiandikisha na kuchagua viongozi bora.
Aidha Munkunda amemuomba Arif kuwaunga mkono madiwani wenzake ili kuhakikisha ligi hiyo inazinduliwa kila kata ndani ya wilaya ya Mtwara na kufikia lengo lililokusudiwa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya Nashiri Pontiya amempongeza Diwani Arif kwa kutekeleza ilani ya chama hicho inayowataka kuinua sekta ya michezo ukizingatia michezo ni sehemu ya ajira hivyo kutokana na ligi hiyo wapo wachezaji ambao wataonekana na wadau mbalimbali na kwenda kucheza klabu kubwa zilizopo nchini.
Naye Diwani wa kata ya Mayanga Arif Suleiman Premji amesema anaungana na serikali kwa ajili ya kuelimisha jamii kwenye upande wa kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura pamoja na kupiga kura, na ameongeza kuwa amepokea maagizo ya Mkuu wa wilaya hiyo na atakaa na kamati yake kuratibu kisha kupeleka kwa mkuu wa wilaya na serikali ikibariki ili ligi hiyo iwe ya wilaya nzima ya Mtwara.