Latest Posts

LISSU ATANGAZA KUMKABILI RAIS SAMIA UCHAGUZI MKUU 2025, AKANUSHA KUGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI CHADEMA TAIFA

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara Tundu Lissu ametangaza kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani (2025), ambapo inadaiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye anayeweza kuwa mpinzani wake wa karibu kwenye nafasi hiyo

Akizungumza na wanahabari leo, Ijumaa Julai 26.2024 kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea mapumzikoni nje ya nchi Lissu amesema bado ana dhamira ya kurejea kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kufanya hicho kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi mkuu uliopita (2020) ambapo mpinzani wake wa karibu alikuwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli (aliyekuwa mgombea wa CCM kwenye uchaguzi huo na mtetezi wa kicho)

Akizungumzia joto la kisiasa lililopo nchini hususani kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu (2024) na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani (2025) Lissu ameeleza utayari wa chama CHADEMA kusimamisha wagombea na kuwaombea ridhaa kwa wananchi wakati utakapowadia, ingawa ametumia nafasi hiyo kutoa tahadhari kwa mamlaka mbalimbali zinazosimamia chaguzi hizo kufahamu kuwa chama hicho hakitakubali kushuhudia yaliyotokea kwenye chaguzi zilizopita (2024 na 2025) zikijitokeza kwenye chaguzi zijazo

Kuhusu uwepo wa mvutano/mgogoro ndani ya chama hicho unaodaiwa kumuhusisha yeye (Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti CHADEMA Tanzania Bara) na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Freeman Mbowe amesema hakuna mvutano au mgogoro wowote kati yao na kwamba mara kadhaa amewahi kutolea ufafanuzi kuwa hana dhamira yoyote ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa katika uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea kama ambavyo wengi wanadai.

Aidha, Tundu Lissu amegusia kauli zinazotolewa na aliyekuwa kada wa chama hicho aliyehamia Chama cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni Mchungaji Peter Msigwa hususani kuhusu madai ya matumizi ya raslimali fedha, utawala bora ndani ya CHADEMA nk, ambapo katika majibu yake Lissu amesema ni jambo la kawaida kuona mtu yeyote aliyekuwa kiongozi mwandamizi pale anapohama kutoa tuhuma kama hizo ambazo kimsingi hazina uhalisia.

Hata hivyo, Lissu amekiri kuwa licha ya kwamba tuhuma hizo hazina uhalisia lakini ni vyema CHADEMA kupitia ofisi ya Katibu Mkuu ikaja na majibu ya kila hoja ili kuondoa sintofahamu na maswali miongoni mwa wanachama na Watanzania kwa ujumla wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!