Latest Posts

LISSU: TUNAENDA KUKINUKISHA, TUTAZUIA UCHAGUZI HUU

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameendelea kusisitiza kuwa chama hicho hakitashiriki uchaguzi wowote hadi kufanyike maboresho ya mfumo wa uchaguzi, akibainisha kuwa msimamo wa No Reforms, No Election si suala la mabishano, bali ni uamuzi wa chama uliopitishwa na vikao vyake vya juu.

Akizungumza Alhamisi, Aprili 3, 2025, katika kikao cha watia nia wa ubunge wa CHADEMA kilichofanyika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam, Lissu amesisitiza kuwa yeyote anayependekeza kushiriki uchaguzi bila mageuzi ya msingi hana mtazamo wa dhati kuhusu hali halisi ya kisiasa nchini.

“Mtu yoyote aliyeshiriki kwenye uchaguzi wetu akakutana na hayo [vitendo vya ukiukwaji wa haki kwa wapinzani] na bado akasema twende tuu, huyo hayuko serious. Uchaguzi wa Tanzania sasa hivi ni machinjioni. Tuliposema No Reforms, No Election kwenye mkutano wa Kamati Kuu hatukua tunatania, tulimaanisha kuwa kama hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi,” amesema Lissu.

Lissu amefafanua kuwa msimamo huo haukuibuka ghafla bali ulipitishwa rasmi na vikao vya juu vya chama, ukiwa ni azimio lililopitishwa na Kamati Kuu chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, na baadaye kuthibitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA Januari 20, 2025, na hatimaye kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa.

“Msimamo wa chama ulipitishwa na Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti Mbowe. Wakati huo mimi nilikuwa Makamu Mwenyekiti, na kwa Katiba hii, Mkutano Mkuu ukisema twende hivi, ni chombo gani kingine kinaweza kupinga? Wote tunataka kuchaguliwa, lakini kwa hali ilivyo hilo haliwezekani bila reforms,” amesisitiza Lissu.

Akiendelea kufafanua msimamo wa chama, Lissu amebainisha kuwa wanachama wa CHADEMA ambao wana matumaini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitabadilika na kuendesha uchaguzi wa haki wanajidanganya. Ameongeza kuwa chama hicho kiko tayari kupambana kwa hali yoyote, huku akitahadharisha kuwa uchaguzi ujao hautakuwa wa kawaida.

“Kwa hiyo tunaenda kukinukisha, walio tayari tutaenda nao, hamna mtu atawekewa bunduki hapa. Wanaofikiri CCM watakuwa wamebadilika, tutawatakia kila la heri. Sanasana huu uchaguzi tutauvuruga huu,” amesema Lissu.

Aidha, Lissu amesisitiza kuwa maandamano na presha ya kisiasa dhidi ya mfumo uliopo ni njia pekee ya kufanikisha mabadiliko, akisema kuwa licha ya hatari zinazoweza kujitokeza, anaamini kuwa mapambano ya ukombozi wa kisiasa yatashinda.

“Kama ulifikiria kuwa Mbunge Novemba, utajichanganya kwa sababu tunaenda kukinukisha vibaya sana, na tutaumia ni kweli, ila nina imani tutashinda. Kwani watatuua? Nikikamatwa nitashtakiwa kwa uhaini kwa kuhamasisha maasi kwenye siasa za ukombozi,” amesema.

Matamshi haya yanaendelea kuonesha msimamo wa CHADEMA wa kutoshiriki uchaguzi wowote bila kufanyika kwa maboresho makubwa ya mfumo wa uchaguzi, huku yakizidi kuchochea mjadala wa mustakabali wa demokrasia nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!