Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu), William Lukuvi, ameishukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kutoa msaada wa dola za Kimarekani 200,000 (Tsh. milioni 532) ili kusaidia juhudi za kurejesha hali baada ya maafa makubwa yaliyotokea Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara.
Lukuvi ametoa shukrani hizo Novemba 12, 2024, katika ofisi za Waziri Mkuu jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa msaada huo ni muhimu katika juhudi za serikali za kufanikisha ujenzi wa shule, vituo vya afya, na soko katika maeneo yaliyoathirika.
Akizungumza wakati wa kupokea mchango huo kutoka kwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub Committee on Refugees, Returnees, and IDPs), Lukuvi ameeleza kuwa Tanzania ilikumbwa na athari za El-Niño mwaka 2023/2024, zilizochangia mafuriko, upepo mkali, na maporomoko ya tope wilayani Hanang.
“Maporomoko ya tope wilayani Hanang yaliathiri maisha ya watu na miundombinu muhimu, ambapo watu 89 walipoteza maisha na wengine 139 walijeruhiwa. Tathmini inaonesha kuwa nyumba 261 ziliathirika, 95 kati ya hizo zilibomoka kabisa,” amefafanua Lukuvi.
Ameongeza kuwa serikali imefanya jitihada kubwa za kukabiliana na maafa hayo kwa kujenga nyumba 108 za makazi kwa waathirika, ambapo nyumba 73 zimejengwa kwa fedha za serikali na 35 kwa msaada wa Shirika la Msalaba Mwekundu.
Aidha, Lukuvi amebainisha kuwa ujumbe wa AU unatarajiwa kutembelea wilaya ya Hanang’ tarehe 14 Novemba, 2024, ili kushuhudia juhudi za serikali na wadau katika kurejesha miundombinu kama vile barabara, umeme, na maji.
Kwa upande wake, Balozi Tabelelo Alfred Boang ameeleza kuwa Kamati ya Mabalozi imeagizwa kufanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza ili kusaidia jitihada za serikali ya Tanzania katika kurejesha hali.
“Muhimu zaidi kama Umoja wa Afrika, kila kidogo tunachochangia ni kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazozikabili nchi za Afrika,” amesisitiza Balozi Boang.