Latest Posts

M/KITI CHADEMA MBARALI: UCHAGUZI WA CHADEMA TAIFA TUNAHITAJI KIONGOZI ATAKAYEONDOA RUSHWA

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Kuelekea uchaguzi wa Taifa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mwenyekiti wa Chama hicho jimbo la Mbarali mkoani Mbeya Peter Mwashiti, amesema CHADEMA inahitaji kiongozi asiye na uoga na mwenye kuthubutu ili kusimamia katiba yake na kukiendeleza Chama hicho kuwa wapinzani wa kweli katika kukemea maovu ndani ya chama na Serikalini kwa ujumla.

Mwashiti amesema hayo Desemba 10, 2024 wakati wa mahojiano yake maalumu na Jambo Tv wilayani Mbarali kuelekea uchaguzi wa chama hicho ngazi ya Taifa baada ya kumalizika katika kanda chache zilizosalia.

Mwenyekiti huyo wa jimbo la Mbarali ambaye pia alikuwa anagombea nafasi ya mkoa wa Mbeya ndani ya chama hicho, amemshukuru mwenyekiti wake wa CHADEMA Taifa Freeman Aikael Mbowe kwa uongozi wake wa kuelekea miaka ishirini sasa akisema CHADEMA pamoja na mapito mengi bado CHADEMA imeendelea kubaki kuwa moja.

Kuhusu aina ya kiongozi ambaye anatarajiwa na wengi ndani ya CHADEMA kwenye uchaguzi ujao, kiongozi huyo amenukuliwa akisema naye amesikia na kuona mitandaoni kuwa Makamu mwenyekiti wa Taifa upande wa bara Tundu Lissu ana mpango wa kugombea nafasi ya uwenyekiti wa Taifa ambapo ameonyesha kukubaliana naye na kudai CHADEMA inahitaji kiongozi ambaye atajidhatiti kukemea Rushwa ambazo zimekuwa zikisikika ndani ya chama hicho.

“Mimi ni muumini wa mabadiliko na nasema Lissu yuko sahihi na anaweza kutufikisha mahali ambapo tunaona tumekwama hasa haya mambo ya Rushwa, Chama chetu (CHADEMA) kinaonekana katika mfumo wa makao makuu umeshindwa kudhibiti mambo kama hayo (Rushwa ndani ya Chama)”, amesema Peter Mwashiti mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Mbarali na kuongeza.

“Uongozi wetu (Taifa) pengine umeshindwa kudhibiti Rushwa na kama tusipoziba ufa tutaenda (siku za usoni) kuwa chama cha watoa Rushwa hata kuliko CCM. Kwahiyo tunataka sasa viongozi wetu tunaoenda kuwachagua waweze kudhibiti mianya ya Rushwa inayoikimbilia CHADEMA ikifika chaguzi wajumbe wasafirishwe na Chama kama tulivyofanya Mbarali mkoa wanajua na kanda wanajua na sio mgombea asafirishe wajumbe. Tukirudi saa hizi watu hata imani imepungua kidogo watu wanaogopa hata kugombea nafasi lakini kuna mambo mengi ya kuchafuana, maadili hamna kwenye Chama chetu (CHADEMA) leo hii ukionekana unasema mambo kama haya wanaanza kusema huyo ni CCM maana yake hata uhuru wa kutoa maoni ndani ya Chama chetu umepungua maana ukisema hili ni kosa wanasema huyo ni CCM au ametumwa na CCM, kwahiyo hatutaki kufika huko tunataka watu wakosoe, sasa tunataka turudi kwenye Chama ambacho tulikuwa tunasema hiki si sawa hiki ni sawa”, ameeleza mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Mbarali Peter Mwashiti.

CHADEMA tangu miaka ya 1995 kimepita katika mitikisiko kadhaa hasa ikihusishwa na baadhi ya vigogo wake kutaka kugombea nafasi ya juu ya Chama hicho kuonekana wana makandokando kana kwamba uenyekiti wa Taifa ni kwa ajili ya watu fulani jambo ambalo linadaiwa kuwa limekuwa likileta shida ndani ya Chama je kuelekea uchaguzi huo wa CHADEMA Taifa ikiwa mwenyekiti wa sasa wa Taifa na makamu wake upande wa bara watagombea wote haiwezi kuleta makundi yenye kufifisha nguvu ya Chama au mpasuko ndani ya Chama? Tumemuuliza mwenyekiti wa jimbo la Mbarali kupata maoni yake na akajibu kuwa;

“Mimi sioni dalili za mpasuko wa CHADEMA, kwanza niwahakikishie wa-Tanzania tuache uoga tunapokwenda kwenye mabadiliko, tunaona Chama Cha Mapinduzi wanapotafuta mgombea wa u-Rais idadi huwa wanafika mpaka arobaini au hamsini mpaka unaamini kabisa kuwa pengine CCM kitapasuka lakini nirudi kwa mwaka huu (2024/2025), Chama chetu kimekua na wana CHADEMA tusiogope mabadiliko eti kwasababu Chama kitapasuka hapana, ni kweli yakitokea makundi mawili ya wagombea sina uhakika sana hao wagombea wawili wanaotajwa (Freeman Mbowe na Tundu Lissu) kama watagombea lakini hata wakigombea naamini hakutakuwa na mpasuko wowote ila kunaweza kukawepo makundi kwasababu kutakuwa pande mbili upande wa mwenyekiti Mbowe na upande wa makamu Tundu Lissu lakini uchaguzi ukipita tukapata mwenyekiti wa Chama tutarudi pamoja kuendeleza jukumu la chama chetu na CHADEMA ni moja”, ameongeza Mwashiti.

CHADEMA ambacho ni Chama kikuu cha upinzani (Tanzania bara) kinakamilisha uchaguzi katika kanda ambazo bado na baadaye kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa viongozi wa Taifa hususani kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2025 ambapo mnyukano mkali unatarajiwa kushuhudiwa kati ya mwenyekiti wa sasa wa CHADEMA Taifa Freeman Aikael Mbowe na makamu wake upande wa bara Tundu Antipas Lissu Mugwai ikiwa wawili hao watagombea kwani mpaka sasa hakuna aliyetoka hadharani kuonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ambayo imeanza kuonekana kwa baadhi ya wanachama na viongozi katika maeneo mbalimbali isipokuwa chaguzi za kiserikali mpaka sasa Tundu Lissu tayari ameshatia nia ya kugombea nafasi ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuandika barua kwa Katibu mkuu wa CHADEMA Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!