
Kituo cha Uwekezaji nchini Tanzania (TIC) chini ya Mkurugenzi mtendaji wake Gilead Teri kimefanikisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji (Tanzania Electronic Investment Window – TeIW), ambao ulizinduliwa mwezi Septemba 2023. Mfumo huu unalenga kurahisisha huduma za uwekezaji nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Â
Awamu ya kwanza ya TeIW imeunganisha mifumo ya Taasisi saba muhimu ambazo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na Kituo cha Uwekezaji (TIC).
Â
Kupitia mfumo huu, mwekezaji anaweza kusajili mradi na kupata vibali vya uwekezaji ndani ya siku tatu tu ikiwa ametimiza vigezo, popote alipo ndani au nje ya nchi.
Â
Katika awamu ya pili ya mradi huu, taasisi nyingine saba zitaunganishwa ili kuboresha zaidi huduma kwa wawekezaji. Taasisi hizi ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Kilimo, Tume ya Madini, na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA).
Â
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, wa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji, huku ikiongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.