Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya ametoa ahadi ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa niaba ya watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji hilo kwa lengo la kuhakikisha linatimiza malengo yaliyowekwa na serikali kuu chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mabelya ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa watumishi wa Jiji waliopandishwa vyeo kwa mwaka 2024 ambapo Bi. Aisha Iddi Ally alikabidhiwa tuzo ya usimamizi bora wa zoezi hilo, pamoja na zawadi ya shilingi milioni moja taslimu.

Mabelya alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa jitihada zake za kuhakikisha watumishi 4,900 wa Halmashauri hiyo wanapandishwa vyeo.
“Natoa shukrani zangu kwa Mhe. Rais kwa niaba ya timu yote ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Tunamtakia heri katika kazi zake kwa sababu amekuwa akiwekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha tunapata mazingira bora ya kazi,” alisema Mabelya.
Pia aliwasihi watumishi wa Halmashauri hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kufuata taratibu za kiutumishi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili.
