Hatua ya ujenzi wa mabweni katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo katika halmashauri ya manispaa ya Iringa ni ukombozi mkubwa kwa wanafunzi wanaolazimika kuishi nje ya chuo na kukumbana na changamoto mbalimbali za kiusalama.
Ujenzi huo unaofanyika kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), umelenga kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, na kwa sasa umefikia asilimia 53 ya utekelezaji wake.
Mabweni hayo yanatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi, hasa wa kike, ambao mara nyingi wamekuwa wakikumbwa na unyanyasaji na usumbufu katika makazi ya nje ya chuo.
Kupitia mabweni hayo, wanafunzi wataishi katika mazingira salama, yaliyo karibu na huduma muhimu za chuo, jambo linalochochea utulivu wa kimasomo na kijamii.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa , kaimu Mkuu wa Chuo alisema kukamilika kwa mabweni hayo pamoja na baadhi ya majengo mengine kutaliwezesha chuo kuongeza idadi ya wanafunzi watakaodahiliwa kila mwaka.
“Kwa sasa tunalemewa na uhaba wa miundombinu ya malazi, lakini mradi huu utaleta mapinduzi makubwa katika uwezo wetu wa kuhudumia wanafunzi,” alibainisha.
Kamati ya Siasa ya Mkoa ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Daudi Yasini imepongeza juhudi hizo, ikisisitiza kuwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuboresha mazingira ya elimu na kulinda ustawi wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Kwa wanafunzi wa MUCE, mabweni haya si tu sehemu ya kulala, bali ni kimbilio la usalama, faraja, na msingi wa mafanikio yao ya kitaaluma alisema mwenyekiti wa ccm mkoa wa Iringa.