Kambi ya tiba ya madaktari Bingwa kutoka Tanzania nchini Comoro imeanza kwa mwitikio mkubwa wa raia wa nchi hiyo ambapo mamia wamejitokeza kupata huduma mbalimbali zinazotolewa kwa ushirikiano na madakatari wazawa katika Kisiwa cha Ngazidja.
Madaktari hao wa Tanzania wametoa huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya mifupa, figo na kibofu cha mkojo, mifupa, saratani, moyo na mengineyo ambapo takriban wagonjwa 417 wameandikishwa katika siku ya kwanza.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya uendeshaji wa kambi hiyo inayoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kaimu Mkuu wa Msafara, Dkt. Salehe Mwinchete ameeleza kuwa ushirikiano waliopewa na madaktari wenyeji ni mkubwa na wananchi wa Comoro wamejitokeza kwa wingi, hivyo kuwatia moyo kuwa siku zinazofuata hali itakuwa bora zaidi.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Comoro Said Yakubu amewaeleza madaktari hao kuwa Kambi Tiba hiyo imekuwa kivutio kikubwa na wananchi wengi wana imani kuwa katika kambi zijazo fani nyingine za afya zitaingizwa.
Kambi hiyo itakayohitimishwa tarehe 4 Desemba,2024 inashirikisha madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali za Benjamin Mkapa, Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).