Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika halmashauri ya wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Mbunge wa Jimbo la Chemba Mohamed Monni amekabidhi madawati 200 kwa shule sita za msingi zikijumuisha shule za Mapango, Chinika, Kelema Kuu, Paranga, Rofati na Chukuruma.
Mbunge huyo amekabidhi Madawati hayo Alhamisi Agosti 8, 2024 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo.
Akikabidhi madawati hayo yenye thamani ya Shilingi milioni 20 Mbunge Monni amesema madawati hayo yatasaidia kupunguza uhaba huo wakati serikali ikifanya jitihada za kumaliza changamoto hiyo
Amesema madawati hayo yatakuwa chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi huku akiwataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu katika kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na wimbi la umasikini katika jamii ya watu wa Chemba.
“Leo nimekabidhi madawati 200 kwa ajili ya shule sita za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Chemba pamoja na jitihada za serikali kupambana na kuboresha miundombinu ya elimu, niwaase vijana wangu msome kwa bidii, elimu ni msingi wa maisha lakini pia ndiyo chanzo kikuu cha maarifa”, ameeleza Monni.