Na Amani Hamisi Mjege.
Wakili tajika nchini Tanzania Peter Madeleka ameelezwa kusikitishwa na mfumo wa haki jinai nchini humo akiutaja kusababisha wananchi wengi kukosa haki akitumia mfano wa kesi aliyokuwa akimsimamia Paul Kisabo dhidi ya Fatma Kigondo, maarufu kama “Afande,” ili kufafanua namna mfumo huo ulivyo.
Katika mazungumzo kupitia jukwaa la Kumekucha la mtandao wa Clubhouse, Jumamosi Oktoba 19, 2024, Madeleka ameeleza kuwa lengo la kushiriki katika kesi hiyo ilikuwa ni kuonesha kwa vitendo jinsi mfumo wa haki jinai unavyokuwa na matatizo makubwa.
“Wananchi wameendelea kuteseka tu kwa sababu haki haipatikani hasa haki jinai, na mimi ni mmoja kati ya wahanga wa mfumo wa haki jinai nchini,” alisema Madeleka.
Ameeleza kuwa walikuwa na uhakika tangu awali kuwa mfumo ulikuwa mbovu, na walitaka kuthibitisha ufanisi wa ripoti ya Tume ya Rais ya Haki Jinai.
“Sasa sisi tulikwenda mahakamani tukijua kabisa tayari mfumo ni mbovu, na tutakapokuwa tukishinikiza mabadiliko ya huu mfumo ni lazima tuwe na mifano hai kwamba huo ubovu mnaousema nyinyi ni ubovu gani,” amesema Madeleka, akiongeza kuwa kesi hiyo ilikuwa mfano halisi wa namna mfumo wa haki unavyokwamisha upatikanaji wa haki.
Katika kesi hiyo, Paul Kisabo alimlalamikia Fatma Kigondo kuratibu kumbaka na kumlawiti kwa kundi Binti wa eneo maarufu la Dar es Salaam kama Yombo Dovya, na mnamo Oktoba 15, 2024, Wakili wake Peter Madeleka aliiomba mahakama kusaini malalamiko hayo ili yawe hati rasmi ya mashtaka. Hata hivyo, Ijumaa Oktoba 18, 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ilitupilia mbali malalamiko hayo, ikieleza kuwa yalikuwa na dosari kadhaa za kisheria, na hivyo kutokidhi vigezo vya kusainiwa.
“Kuna njia ambazo mtu yeyote anaweza kuyapeleka malalamiko yake kwa hakimu kisheria, na yapo kwa njia mbili; ya mdomo na ya maandishi. Sisi tumepeleka kwa njia ya maandishi, lakini hakimu akasema hayo maandishi ni defective (Yenye kasoro),” amesema Madeleka.
Amefafanua kuwa chini ya Kifungu cha 128(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hakimu akishapokea malalamiko anatakiwa kutengeneza hati ya mashtaka. Hata hivyo, hakimu aliangazia dosari za kisheria badala ya kuandaa hati ya mashtaka, hali inayoashiria kuwepo kwa ‘kigugumizi kikubwa’ cha kumkamata Fatma Kigondo maarufu “Afande.”
Madeleka ameongeza kuwa licha ya changamoto walizokutana nazo, walifanikiwa kwa namna fulani kuonesha kile alichokiita ubovu wa mfumo huo wa haki jinai.
“Kesi yetu ilipofunguliwa, ndiyo polisi wakasema jalada la upelelezi la Afande limeshakamilika na lipo kwa DPP. Lakini mpaka sasa, DPP hajachukua hatua yoyote kuhakikisha haki ya yule binti inapatikana kwa kumkamata Afande na kumpeleka mahakamani,” amesema Madeleka.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, uliotolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Nyambuli Tungaraja, ulionesha kuwa Kigondo hatokabiliwa na mashtaka yoyote dhidi yake kwa sasa. Hata hivyo, Wakili Madeleka amebainisha kuwa matokeo ya kesi hii yameonesha wazi kuwa mfumo wa haki jinai ni mbovu na unahitaji mabadiliko makubwa.
“Katika hili, sisi tunatembea kifua mbele kwa sababu tumefanikiwa kuthibitisha kwamba kweli hata wenzetu, akina Jaji Othman Chande, walichokuwa wakisema kuhusu mfumo wa haki jinai ni sahihi. Mahakama inaangalia sura, polisi inaangalia sura nani amefanya kosa wamkamate, na DPP anaangalia sura,” amesema Madeleka kwa msisitizo, akionya kuwa haki haipaswi kutolewa kwa upendeleo au kuzingatia cheo au nafasi ya mtu katika jamii.