Na Josea Sinkala, Mbeya.
Madereva wa Kampuni ya China Henan International Coorporation Group Co. Limited (CHICO) inayotekeleza mradi wa barabara ya njia nne mkoani Mbeya, wamesitisha utoaji huduma ya usafirishaji bidhaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakilalamikia stahiki zao lukuki ikiwemo ukosefu wa mikataba hatua iliyowafanya wasitishe kuendelea na kazi Mei 13, 2025.
Wakizungumza mapema Mei 13, 2025, baadhi ya madereva hao wamesema wameingia kwenye mgomo huo kutokana na kwamba wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu ya kutokuwa na uhakika na usalama wa kazi yao.
Wamesema baadhi ya kadhia zinazowakabili ni pamoja na makato ya mfuko wa hifadhi ya jamii isivyo halali, baadhi ya madereva kukosa mikataba stahili ya kazi na kukatwa upotevu wa mafuta ya magari hivyo kukwamisha utendaji kazi kutokana na jiografia ya mkoani Mbeya kuwa ya milima na mabonde.
Wamesema mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne unaonekana kusuasua kutokana na madereva kutothaminiwa hususani kukosa stahiki zao ipasavyo, malalamiko ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu (kuanzia miezi nane hadi miaka miwili) hivyo kuiomba Serikali hasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati madai yao ili kupata stahiki zao.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, afisa raslimali watu wa mradi huo amekanusha madai hayo akisema kampuni ya Chico ilishawapa mikataba madereva hao na madai yao mbalimbali hasa utoaji wa mafuta yapo kwenye mikataba yao.
Serikali ya Tanzania inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne ambapo kwa hatua ya sasa inatoka Nsalaga Uyole hadi Ifisi Mbeya vijijini (Kilomita 29) ambapo pamoja na kuendelea kwa ujenzi huo mara kadhaa umekuwa ukisuasua huku sababu zikihusishwa na upungufu wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi ambapo sasa ujenzi unaonekana kuendelea katika maeneo kadhaa jijini Mbeya hivyo ni vema tofauti kama hizi zikatazamwa kwa jicho la tatu ili kuharakisha mpango wa Serikali kuona barabara hiyo inakamilika kwa wakati ili kuchochea maendeleo kwa wananchi.