Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, limewapongeza wanafunzi wa darasa la saba kwa kufanya vizuri na kuazimia kianzisha programu za mitihani ya wiki ikiwa ni mkakati wa kupandisha ufaulu wilayani humo.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani kwa ajili ya kupokea taarifa za Kata, Mwanyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi George Musyani, amesema jitihada zilizofanywa na wataalamu kupandisha ufaulu zinatakiwa kutiliwa mkazo ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Tutengeneze mkakati ambao tutakwenda nao mpaka mwakani ili watoto wetu wafaulu zaidi. Nawashukuru walimu kwa jitihada zao zilizowafanya wanafunzi hao (wa Mbozi) kuongeza ufaulu kutoka asilimia 74 mpaka asilimia 81”, amesema Musyani na kuongeza;
“Twendeni kuanzisha programu za mitihani ya kila mwisho wa wiki ambayo inaweza kufanyika kwa kushindanisha shule kwa shule ambayo itawafanya wasome kwa bidii. Tujitahidi kwenda kutoa elimu kwa wananchi wetu kuhusiana na suala hili ili wote tuwe na uelewa wa pamoja ili kusitokee manung’uniko ndani ya jamii”, amesisitiza.
Pia Musyani ambaye ni Diwani kata ya Nanyala, amewataka madiwani hao kwa kushirikiana na watendaji, waratibu elimu kata pamoja na polisi kata kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanajiunga na masomo ya sekondari.
Akichangia katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Bara Mhe. Alois Mndalavuma, ameishauri Halmashauri hiyo ianze mpango wa ujenzi wa mabweni ili kudhibiti utoro wa wanafunzi.