Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Mtwara mjini wametakiwa kuwa wapole, kuheshimu wananchi na kutokuwa waoga kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Mtwara Mjini, Salumu Naida wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vipaza sauti vitakavyowasaidia wagombea hao kipindi cha kampeni kwa wagombea wa uchaguzi huo.
Aidha amewaagiza wagombea hao kutoa taarifa sahihi ili kufanya uchaguzi huo uwe huru na rahisi na kusiwe na taarifa za kubuni kwa ajili ya maslahi binafsi, na wahakikishe wanapokea taarifa kutoka kwenye Kamati ya siasa ya Wilaya, kata na tawi na kuacha kupokea taarifa kwa watu wasiokuwa kwenye kamati za siasa.
Amewataka madiwani wa kata zote jimboni humo kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo kwani hawatokuwa tayari kutoa fomu kwa Diwani ambaye hataki kujitoa kwenye uchaguzi huu.
“Makatibu tunahitaji madiwani ushiriki wao kwenye uchaguzi huu na kama hashiriki hatakama ni rafiki yako usimung’unye maneno” Amesema Naida.
Ameongeza ”Tutawapimeni kwa kazi mnazoweza kutufanyia, asitokee Diwani mwengine hashiriki kitu chochote alafu mkaficha maovu yake mana diwani si wakuja kuangalia tu yeye ni rasilimali fedha kwetu sisi katika kata zetu lazima wachangie.”
Sambamba na hilo Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amekabidhi vipaza sauti kwenye kata 8 na kutoa pesa taslimu kwa ajili ya kukodi vipaza sauti kwa kata nne ambazo hazijapata vipaza sauti lengo likiwa ni kujiandaa na uchaguzi huo.
Jumla ya kiasi cha shilingi milioni 15 zimetumika kwa ajili ya kununua vipaza sauti ili kuwasadia wagombea hao kwenye kipindi hicho cha kampeni.