Maelfu ya wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali mkoani Dodoma, wanaoshiriki katika Kampeni ya Mama Asemewe, wamefanya matembezi maalum kwa ajili ya kuweka maazimio kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Matembezi hayo yaliyofanyika siku ya Jumamosi yameongozwa na Mwenyekiti wa Kampeni ya Mama Asemewe, Geofrey Kiliba, yakihusisha wanachama wa kampeni hiyo wanaounga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya matembezi hayo, Geofrey Kiliba ameeleza kuwa lengo ni kuonesha mshikamano wa wanavyuo katika kuchagiza maendeleo ya taifa na kuandaa mikakati ya kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao.
“Tunatambua mchango wa vijana katika ustawi wa nchi yetu, na kupitia Kampeni ya Mama Asemewe tunajipanga kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika kujenga Tanzania yenye maendeleo endelevu chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Kiliba.
Katika maazimio yao, wanavyuo wamesisitiz kushiriki kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi, kuhakikisha ushiriki wa vijana katika siasa unakuwa na nguvu na kueneza uelewa kuhusu sera na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Baada ya matembezi hayo, kongamano kubwa la wanavyuo limefanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, likiwakutanisha wanavyuo, viongozi wa kampeni hiyo, na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Deogratius Ndejembi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo mipango zaidi iliwekwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kampeni ya Mama Asemewe imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wanavyuo wanaounga mkono maendeleo ya Tanzania. Kupitia kampeni hii, vijana wanahamasishwa kushiriki katika mijadala ya kitaifa, kuelewa sera za maendeleo, na kuhakikisha sauti zao zinasikika katika masuala ya kisiasa na kijamii.