Mafunzo kwa askari wa kike ukanda wa Afrika (IAWP) yamefunguliwa siku ya Jumanne Julai 02, 2024 katika kituo cha Rasilimali ya Polisi Abuja nchini Nigeria yakilenga kuwajengea uwezo askari wa kike ukanda wa Afrika na wasimamizi wa sheria.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Rais wa Shirikisho la Askari wa Kike Duniani Dkt. Leah Shibambo’s ameshukuru shirikisho la wakuu wa Polisi kwa namna ambavyo wamekuwa na ajenda za kuongeza nafasi za wanawake katika ajira na mgawanyo wa majukumu.
Ameongeza kuwa kitendo cha wakuu hao wa Polisi kuwa na ajenda za kuwajengea uwezo wanawake imeongeza kujiamini kwa kundi hilo katika utekelezaji wa majukumu yao huku ikileta matokeo chanya katika kutoa huduma bora katika jamii.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Nigeria IGP Phd. Kayode Egbetokun amesema kuwajengea uwezo askari wa kike umewasaidia na kufanya askari hao kujituma katika kazi na kujiamini kitendo kilicholeta matokeo chanya katika jamii huku akibaisha kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi ambapo dunia imejikita katika usawa wa kijinsia.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi kutoka nchini Tanzania Dkt. SACP Debora Magiligimba ambaye ni mjumbe kutoka Tanzania amebainisha kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wake Mrakibu wa Idara ya Uhamiaji kutoka nchini Ghana SI Doris Hajiman amebainisha kuwa maandalizi ya mafunzo hayo ni mazuri huku akiwapongeza waandaji wa mafunzo hayo ambao ni nchi ya Nigeria.