Latest Posts

MAGEREZA UNGUJA NA PEMBA KUANZA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, amefanya mazungumzo na Kamishna wa Magereza Zanzibar, Khamis Khamis, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ya Rafiki Briquettes, badala ya kuni na mkaa.

Mazungumzo hayo yalilenga kufanikisha azma ya magereza visiwani Zanzibar kubadili mfumo wa matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati hiyo safi na salama. Dkt. Mwasse alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia nchini.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mwasse pia alikutana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dkt. Islam Salum, ambapo walijadili namna ya kufikisha nishati safi ya Rafiki Briquettes kwa jamii visiwani Zanzibar. Mazungumzo hayo yaliangazia pia utekelezaji wa Sera ya Nishati Safi na Salama, ambayo inalenga kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Kwa upande wake, Kamishna wa Magereza, Khamis Khamis, aliishukuru STAMICO kwa kuonyesha nia ya kusaidia magereza kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aliahidi kushirikiana na STAMICO kutekeleza hatua zilizojadiliwa ili kuhakikisha magereza ya Unguja na Pemba yanajumuika katika mpango huo wa matumizi ya Rafiki Briquettes.

Ziara ya Dkt. Mwasse visiwani Zanzibar ilifanyika kufuatia mwaliko wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha visiwa vya Unguja na Pemba vinanufaika na mpango wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!