Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imewahukumu wakazi wa Kijiji Cha Mandang’ombe wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ambao ni Mussa Shija (33) na Hollo Shija (35), kwenda jela miaka 20 na na miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kuzini na maharimu.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 14, 2024 mwaka huu na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Enos Misana katika kesi ya jinai Namba 26634/2024 baada ya washtakiwa kukiri makosa yao.
Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mashitaka ya Taifa wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Vedastus Wajanga ameeleza kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo tarehe na miezi tofauti kati mwaka 2018 hadi tarehe 31/07/2024 katika kijiji cha Mandang’ombe wilayani humo.
Mwendesha Mashitaka huyo aliielezea mahakama kuwa washitakiwa ni ndugu wa damu kwa maana ya kaka na dada na katika uhusiano wao walikuwa wakiishi kama mke na mume huku wakibahatika kupata mtoto mmoja mwaka 2022 ambaye jina lake limehifadhiwa.
Washitakiwa waliomba mahakama iwapunguzie adhabu wakieleza kukosea kwa mara ya kwanza na kuwa na familia inayowategemea, na kwamba walichokifanya hawakujua kuwa ni kosa kwani waliambiwa na babu yao mzaa baba kuwa ili wadumishe mila za ukoo wake wanatakiwa wao waoane.