
Katika jitihada za kupunguza hatari za kiusalama kwa watoto wa kike wanaolazimika kuishi nje ya maeneo ya vyuo, Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa mabweni ya wasichana ili kuwawezesha kusoma katika mazingira salama na tulivu.
Ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli umefikia asilimia 58, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa ya makazi kwa zaidi ya wanafunzi 500 pindi mradi huo utakapokamilika.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo chuoni hapo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema watoto wa kike wako kwenye hatari zaidi wanapolazimika kuishi nje ya maeneo ya chuo, na kusisitiza kuwa kukamilika kwa mabweni hayo kutapunguza changamoto za kiusalama na kuwapa wasichana nafasi ya kusoma kwa utulivu na kuzingatia ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Boniface Daniel, amesema fedha zilizopokelewa hivi karibuni zitawezesha kuingia awamu ya nne ya ujenzi wa mabweni, hatua itakayoharakisha kukamilika kwa mradi huo na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
