Ikiwa siku chache zimepita tangu tulivyoripoti taarifa kuhusu wananchi wa Bondo, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kulia kukosa makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto na kubomolewa kwa kuambiwa wamevamia hifadhi.
Jambo TV imefunga safari na kufika katika maeneo hayo na kushuhudia Maelfu ya wakazi hao ambao wamejikuta wakiishi chini ya miti na vichakani baada ya makazi yao kuchomwa moto.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya kaya 2,600 zimeachwa bila makazi, mali zao kuharibiwa, na familia zao kutawanyika, huku wengine wakiwa hawajui walipo wapendwa wao, ikiwemo watoto wadogo.
Tukio hili linahusishwa na operesheni ya kuwaondoa wananchi hao kwa madai ya kuvamia eneo la hifadhi ya msitu. Kwa mujibu wa mashuhuda, usiku wa tarehe 3 Januari ulikuwa wa mateso yasiyosahaulika, baada ya vikosi vya ulinzi vilivyojihami kwa silaha kuingia eneo hilo na kuanza kuwafurusha kwa nguvu. Inadaiwa kuwa mabomu ya machozi, risasi na moto vilitumika katika kuwaondoa wakazi hao, huku wengine wakidai kupigwa, kuteswa na hata wanawake kubakwa mbele ya watoto wao.
Maisha Yaliyobadilika Ndani ya Usiku Mmoja
Baada ya operesheni hiyo, hali ya wananchi imeendelea kuwa mbaya zaidi. Wengi wao sasa wanaishi bila makazi, mavazi, wala chakula cha kutosha. Wanawake, watoto, na wazee wanalazimika kulala chini ya miti huku wakijifunika vyandarua na mabaki ya magunia kujikinga na baridi kali ya usiku.
Kuna simulizi ya kusikitisha ya mama mmoja ambaye alilazimika kujifungua kichakani wakati wa purukushani hizo. Akiwa katika uchungu wa kujifungua, alikosa msaada wa kitabibu na mazingira salama, hali iliyohatarisha maisha yake na ya mtoto mchanga. Tukio hili linaonyesha ukubwa wa mateso na changamoto wanazokabiliana nazo wakazi wa eneo hilo.
“Hatujui hatma yetu. Hatuna chakula, hatuna mavazi, na hatuna pa kwenda. Watoto wetu wamepotea, wengine wamekufa kwa njaa na mateso. Hii ni Tanzania au tuko vitani kama Burundi au Kongo?” alisema mmoja wa wakazi kwa uchungu mkubwa.
Kilio cha wananchi hao kinazidi kuongezeka baada ya kuzuiwa hata kurejea katika mashamba yao kwa ajili ya kuvuna mazao waliokuwa wameyapanda. Wanadai kuwa wananyimwa hata nafasi ya kuchukua chakula chao, jambo linalowafanya waishi kwa njaa kali.
Tumaini kwa Rais Samia
Katika juhudi za kutafuta msaada, baadhi ya wakazi walifunga safari hadi Dodoma kwa lengo la kuonana na viongozi wa serikali ili kuwasilisha kilio chao. Hata hivyo, juhudi zao bado hazijazaa matunda. Wananchi hawa wanaendelea kuiomba serikali, hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili kupata suluhisho la kudumu kwa mateso wanayopitia.
Elimu Yasimama, Mustakabali wa Wanafunzi Hatihati
Mbali na makazi yao kuteketezwa, shule katika eneo hilo pia zilichomwa moto, jambo lililosababisha wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo yao. Familia nyingi sasa zinajiuliza hatma ya watoto wao, ambao ndoto zao za kupata elimu zimekatizwa ghafla.
Maswali Yasiyo na Majibu
Licha ya kwamba Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batlida Buriani, pamoja na viongozi wengine wa wilaya kueleza kuwa wananchi hao wameondolewa kwa sababu ya kuvamia hifadhi, bado kuna maswali mengi yanayoibuka. Kwa nini operesheni hii ilihusisha matumizi ya nguvu kiasi hiki? Kwa nini watu waliovamia hifadhi walionywa kwa muda mfupi tu kabla ya kuondolewa kwa nguvu? Na kwa nini wananchi wanazuiliwa kupiga picha kwani baadhi yao wanadai kuporwa simu zao pindi tu walipoonekana kutaka kufanya hivyo.
Kwa sasa, maeneo yaliyotangazwa kuwa hifadhi yameshapewa mipaka rasmi na kuwekwa mabango ya amri. Lakini je, ni haki kwa wananchi hawa kufurushwa kwa njia hii bila kupatiwa makazi mbadala?
Hali ya wakazi wa Bondo bado ni tete. Kilio chao kimejaa simanzi, mateso, na mashaka, wakisubiri suluhisho kutoka kwa viongozi wa kitaifa. Wana matumaini kuwa sauti zao zitasikika na hatimaye haki yao itatendeka.
Nakala hii ni sehemu ya jitihada za kuangazia changamoto zinazowakumba wananchi waliopo pembezoni mwa jamii. Tunatoa wito kwa serikali na wadau wa haki za binadamu kushughulikia suala hili kwa dharura.
Fuatilia kwa undani zaidi kupitia Youtube ya Jambo TV