Latest Posts

MAKALLA AITAKA CHADEMA KUKUBALI MATOKEO IKIAMUA KUSHIRIKI UCHAGUZI

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, amesema kuwa uchaguzi utafanyika hata kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakitashiriki, kwani vyama vingine vingi tayari vimejiandaa kushiriki.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mkoani Iringa Machi 28, 2025, Makalla amesisitiza kuwa CCM inaingia kwenye uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushangazwa na msimamo wa CHADEMA wa kususia uchaguzi kwa madai ya kutaka Katiba Mpya.

“CCM ni chama kikubwa, kinapenda demokrasia na kinaheshimu Katiba ya nchi. Wameamua wao kususia uchaguzi, hatuwalazimishi, lakini vyama vingine vitashiriki na uchaguzi utafanyika bila wao,” amesema Makalla.

Makalla amedai kuwa ndani ya CHADEMA kuna mvutano mkubwa kati ya viongozi na wanachama kuhusu nafasi za udiwani na viti maalum. Amebainisha kuwa chama hicho kiliahirisha mkutano wake wa tarehe 3 Aprili, 2025 kwa lengo la kuitikisa CCM ili waitwe kwenye mazungumzo, lakini hatua hiyo haijabadilisha msimamo wa CCM kuhusu uchaguzi.

“Baada ya kuona tumewapotezea, sasa wamesema watatoa msimamo wa chama kuhusu watia nia. Wamefungwa ndani ya chama chao, lakini vyama viko vingi. Wanaotaka kugombea waende kwenye vyama vingine,” amesema.

Aidha, Makalla amedai kuwa CHADEMA haina mgombea wa urais kwani hakuna anayewaza kushindana na Rais Samia Suluhu Hassan. Amewashauri vijana na wanawake wa CHADEMA wenye nia ya kugombea kutafuta vyama vingine ili kutimiza malengo yao ya kisiasa.

Kuhusu uandikishaji wa wapiga kura, Makalla amesema kuwa viongozi wa CHADEMA waliwaambia wanachama wao wasijiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, jambo ambalo litawafanya wakose nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu.

“Msije kutupigia kelele mkishindwa kwa sababu hamkujiandikisha. Sisi (CCM) tumehamasisha watu na wamejiandikisha, hivyo tunategemea ushindi wa kishindo,” amesema.

Makalla ameongeza kuwa iwapo CHADEMA wataamua kushiriki uchaguzi kwa kuchelewa, hawana sababu ya kulalamikia matokeo kwani walijiondoa kwenye mchakato wa maandalizi.

“Leo mkianza kusema mmefanya maamuzi ya kushiriki uchaguzi, mkishindwa msilalamike. Watu wenu mliwaambia wasijiandikishe, sisi tumehamasisha na tunategemea ushindi mkubwa,” amesisitiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!