Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi mbalimbali hautokani na ujanja au nguvu ya chama hicho, bali ni ridhaa ya wananchi wanaokiamini kutokana na sera zake, mipango na utekelezaji wa maendeleo.
Makalla ametoa kauli hiyo Aprili 16, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Nimesikia baadhi ya vyama wanasema tutashiriki uchaguzi, tumechoka kukiacha CCM kikiendelea kushinda uchaguzi, tumechoka CCM kuendelea kutawala. Jibu langu ni rahisi tu, CCM haijajiweka madarakani kwa nguvu, CCM inapata ridhaa ya wananchi, na hii ni kutokana na kukubalika kwake kwa sera, mipango na kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema Makalla.
Aliwataka vyama vya upinzani vinavyotaka kushindana na CCM kujiandaa kwa kampeni za sera badala ya malalamiko, huku akisisitiza kuwa chama hicho kina mtandao mpana wa wanachama, wafuasi na wapenzi nchini kote.
“Anayedhani kwamba ana uwezo wa kushindana na CCM katika kusaka dola tunamkaribisha, wawe na Ilani, washiriki kampeni, tubishane kwa sera, tuongee majukwaani, wataona nguvu ya CCM… sisi hatujiweki madarakani, tunawekwa madarakani na wananchi kwa imani kubwa waliyonayo kwetu,” aliongeza.
Katika siku hiyohiyo, Chama cha ACT Wazalendo kilitangaza rasmi kuwa hakitasusia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikieleza kuwa kitautumia uchaguzi huo kama uwanja wa mapambano ya kupinga hujuma dhidi ya demokrasia na kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, alitoa tamko hilo katika hotuba maalum iliyotolewa katika ofisi za chama zilizopo Vuga, Zanzibar.
“Baada ya tafakuri ya kina, chama chetu kimejiridhisha kuwa CCM kinahitaji na kwa hakika kitafurahia iwapo vyama makini vya upinzani vitasusia uchaguzi ili kiendeleze hujuma kwa demokrasia nchini. ACT Wazalendo tumegoma kutoa fursa hiyo kwa CCM,” alisema Semu.
Kwa mujibu wa Semu, kususia uchaguzi kumechangia kuimarisha hujuma dhidi ya demokrasia katika nchi mbalimbali duniani, na kwa msingi huo, ACT Wazalendo itaingia kwenye uchaguzi kwa lengo la kulinda misingi ya kidemokrasia na kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.