Latest Posts

MAKALLA: CHADEMA WANA AJENDA YA SIRI KUDHOOFISHA UTAWALA WA SHERIA NCHINI

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amesema uchaguzi mkuu nchini uko palepale kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa harakati zozote za kuupinga hazitaathiri ratiba ya uchaguzi.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Makalla amewashutumu viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akidai kuwa wamekifanya chama hicho kupoteza mwelekeo na sasa kinaelekea kuwa jukwaa la harakati badala ya chama cha siasa chenye lengo la kushika dola.

“CHADEMA baada ya uchaguzi huu watabaki kama jukwaa la harakati, kwa sababu chama cha siasa lengo lake ni kushika dola. Katiba yao ibara ya 4 inasema watashiriki uchaguzi na kushika dola. Kwa sasa, wamepoteza mwelekeo,” amesema Makalla.

Katika hotuba yake, Makalla amekosoa vikali hatua ya baadhi ya viongozi wa Chadema, akimtaja Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kwa kile alichokiita kuwa ni kuhamasisha wafuasi kwenda kwa wingi mahakamani ambako kuna eneo dogo lisiloweza kuhimili umati mkubwa, jambo alilolielezea kuwa ni “harakati zisizo na tija.”

“Hivi katika akili ya kawaida, unawaambia watu wote waende mahakamani – Ubungo, Ukonga, Kawe, Kigamboni – kweli inawezekana? Maeneo yenyewe madogo ya mahakama. Hiyo ni mishemishe ya harakati,” amesema.

Makalla ameendelea kushutumu CHADEMA akidai kuwa chama hicho kipo katika harakati za kuvuruga utawala wa sheria nchini kwa kuingilia kazi za mihimili huru ya dola, ikiwemo mahakama na jeshi la polisi.

“Haiwezekani kuingilia kazi za mahakama, haiwezekani kuzuia jeshi la polisi kutimiza wajibu wake, haiwezekani kueneza uongo na upotoshaji. Lengo lao ni kufanya serikali, mahakama na bunge visifanye kazi vizuri,” amesema Makalla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!