Latest Posts

MAKALLA: VYAMA VYA UPINZANI HAVINA NGUVU YA UMMA YA KUZUIA UCHAGUZI

Katibu wa Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, Amos Gabriel Makalla, amesema hakuna chama chochote chenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi kwa kuwa ni takwa la katiba ya nchi.

Makalla amesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika siku ya Alhamisi katika uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya, akiwa ameambatana na viongozi wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Afrey Nsomba, na kada wa CCM kutoka Iringa, Peter Msigwa.

Katika hotuba yake, Makalla ameeleza kuwa vyama vya upinzani, hususan CHADEMA, vinajinasibu kuwa vitatumia nguvu ya umma kuzuia uchaguzi kufanyika, lakini amedai kuwa hawana nguvu hiyo.

“Hakuna mtu au chama chenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi kwa sababu ni takwa la katiba. Uchaguzi lazima ufanyike na CCM tuko tayari kushinda kwa haki na kwa hoja,” amesema Makalla.

Aliongeza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wa mwaka 2024 ulikuwa ni jaribio la mitambo, huku akisisitiza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utampa CCM ushindi mkubwa kutokana na rekodi yake ya utendaji bora kwa wananchi.

Katika mkutano huo, Makalla pia ameeleza kusikitishwa na tukio la kupigwa kwa Katibu Mwenezi wa BAWACHA Taifa, Siglada Mligo, lililoripotiwa kufanywa na mlinzi mmoja wa CHADEMA. Ameelekeza viongozi wa CCM Mkoa wa Njombe kumtembelea Mligo na kumpa pole kwa tukio hilo.

Akizungumzia suala la Tume Huru ya Uchaguzi, Makalla amesema serikali ilihakikisha tume hiyo inapatikana kwa njia shirikishi tofauti na zamani ambapo Rais wa Nchi ndiye aliyeteua watendaji wake moja kwa moja.

Amewataka wananchi kutosusia uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa sababu tume hiyo sasa ni huru na uchaguzi utakuwa wa haki.

“CCM imejipanga kushinda kwa haki na kwa kishindo, na tunataka kuhakikisha kuwa kata na majimbo yote ya Mkoa wa Mbeya yanachukuliwa na CCM,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, Mchungaji Peter Simon Msigwa, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa CHADEMA kabla ya kuhamia CCM, amewataka wananchi kutosusia uchaguzi kwa kuwa ni njia muhimu ya kupata viongozi wa kuwatumikia wananchi.

Ameisifia serikali ya CCM kwa kusema kuwa ni serikali imara na sikivu inayoshughulikia matatizo ya wananchi kwa vitendo, tofauti na wapinzani ambao amedai hawana suluhisho la matatizo ya wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!