Latest Posts

MAKALLA: WATANZANIA TULINDE AMANI, TANZANIA HAINA MGOGORO WA KISIASA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amewataka Watanzania kulinda amani ya nchi na kusimama pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, akidai kuwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanawatumia wafuasi wao kwa maslahi binafsi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam, Makalla amesema CHADEMA wamepoteza mwelekeo wa kisiasa na sasa wameingia kwenye kile alichokiita “biashara ya kisiasa,” wakifanya harakati zinazowalenga kuwapendezesha wale wanaowatuma kutoka nje ya nchi.

“CHADEMA wanajifanya kama watoto wanaodeka, wakiambiwa wasaini kanuni za maadili ya uchaguzi wanagoma, wakidai wamechoka. Na mimi nakubali kweli wamechoka,” amesema Makalla.

Akizungumzia tukio la baadhi ya wafuasi wa CHADEMA kwenda kushuhudia kesi ya Mwenyekiti wao Tundu Lissu mahakamani, Makalla amedai kuwa viongozi wa chama hicho waliwatuma wafuasi wao kwenda kupambana na vyombo vya dola huku wao wakijificha na kutojihusisha moja kwa moja.

“Baadhi walikwenda mahakamani na kukumbana na vyombo vya dola, lakini viongozi wao walijificha. Katibu Mkuu wao John Mnyika alikiri kuwa hakuguswa mahali popote na hata akasema anaona aibu kusimama mbele ya watu. Lema naye alisema walikuwa wamekaa kimkakati tu,” amesema Makalla.

Ameongeza kuwa hali hiyo inaonesha wazi kuwa viongozi wa CHADEMA wanawaweka wananchi mstari wa mbele kupambana ili wao wafaidike, huku wakipata fedha kutoka kwa watu wanaowatuma.

Makalla amesisitiza kuwa Tanzania ni salama na haina mgogoro wowote wa kisiasa, akisisitiza kuwa mihimili ya dola, ikiwemo mahakama, inapaswa kuheshimiwa na kuachiwa ifanye kazi bila kuingiliwa.

“Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hakuna mgogoro wa kisiasa. Tanzania ni salama,” amesisitiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!