Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Naibu Waziri wa mambo ya nje Ngwaru Maghembe ameomba Serikali kuona namna ya kutatua kero ya uwepo wa wanyama waharibifu hasa tembo wanaoingia katika makazi ya wananchi na kuharibu mazao na wakati mwingine kusababisha vifo.
Ametoa ombi hilo Februari 18,2026 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Wilaya hiyo ambapo amesema tembo wamekuwa ni kero katika Kata za tambarare ambapo wamekuwa wakiharibu mazao, miundombinu ya maji na kuua hivyo kuomba ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuagiza wataalam wa maliasili kufika na mitambo ya kisasa kufuatilia tembo hao na kurudishwa katika hifadhi ufanyike ili kuepusha madhara.
Akijibu changamoto hiyo Waziri wa Maliasili na utalii Dkt.Ashatu Kijaji amesema kuwa tayari teknolojia ya kufunga mikanda kwenye makundi ya tembo ili waweze kufuatiliwa kama alivyoelekeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeshafanyika ambapo mpaka sasa makundi matano ya tembo wamefungwa mikanda yenye teknolojia hiyo na kuwaona kila walipo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu mbali na hilo tumesha nunua ndege nyuki mbili Wilayani Mwanga kwaajili ya kutumia kuwarejesha tembo hifadhini pamoja na kujenga vituo viwili vyenye Askari nane na magari mawili ili kusaidiana na hizi teknolojia kuzuia makundi haya ya tembo kuja kwenye maeneo ya Wananchi wetu” alisema Dkt Kijaji.
Aidha amesema kuwa Wananchi wapatao 1,690 wa Wilaya za Same na Mwanga Mkoani humo wameshalipwa jumla ya shilingi 410,905,000 kama kifuta jasho na kifuta machozi kufuatia madhara ya wanyamapori waharibifu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka watendaji wa TAWA na TANAPA kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama hao kwani maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamesha tekelezwa.
Waziri Mkuu yupo katika wizara ya siku nne Mkoani Kilimanjaro ambapo atatembelea Wilaya zote za Mkoa huo, kukagua miradi mbalimbali pamoja na kuzindua.