Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata na kuwashikilia watuhumiwa nane wanaohusishwa na matukio matatu tofauti ya uhalifu yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi watuhumiwa wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke mmoja pamoja na mtoto wake mchanga wa miezi minne. Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Machi 28, 2026 majira ya saa tisa alasiri katika Kitongoji cha Tawini kwa Mgongo, Kijiji cha Kisangasa, Wilaya ya Kilindi.
Inaelezwa kuwa marehemu Mwajabu Shaban (30) pamoja na mwanawe Mwantumu Abdala waliuawa kikatili kabla ya miili yao kutumbukizwa ndani ya kisima cha maji.
Katika tukio lingine, watuhumiwa wawili wanashikiliwa kwa kumjeruhi vibaya Yassin Amiri, fundi simu mkazi wa Makorora Jijini Tanga, ambapo uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Aidha, Polisi wamewakamata watu wawili waliokutwa na noti bandia 16 zenye thamani ya shilingi 160,000 endapo zingekuwa halali.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa walikuwa wakichanganya fedha hizo na halali ili kujipatia bidhaa na huduma kwa njia ya udanganyifu.
Mbali na matukio hayo ya kihalifu, Polisi pia wametoa taarifa ya ajali ya moto uliosababishwa na mlipuko wa petroli katika Kijiji cha Bongi, Wilaya ya Handeni. Tukio hilo lililosikitisha lilisababisha kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka nane huku watu wengine watatu wakijeruhiwa na kuendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Katika operesheni maalum, Jeshi la Polisi limefanikiwa pia kukamata pikipiki 11 zisizo na namba za usajili, huku uchunguzi ukiendelea kubaini uhalali wake na hatua za kisheria kuchukuliwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewataka wananchi kuendelea kushirikiana nao kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kudumisha amani na usalama katika jamii.