Na; mwandishi wetu
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa vipaumbele 12 vilivyowekwa na mkutano wa nne wa Dunia kuhusu maendeleo ya wanawake uliofanyika Baijing -China mwaka 1995 (miaka 30 iliyopita) umekuwa na mafanikio kadhaa hapa nchini
Hayo yamebainika kwenye hafla ya kushetehekea mafanikio ya Beijing 30+, iliyofanyika, Jumatano Aprili 16.2025, kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambapo imetajwa kuwa mafanikio hayo yamebanishwa kufuatia mtandao wa wanaharakati wanawake kuandaa hafla hiyo huku ikijikita kufanya tathmini kwa kuangalia Katiba, uchaguzi na uongozi
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari kuhusu tukio hilo, imebainisha kuwa vipaumbele hivyo 12 vya Beijing ni pamoja na Wanawake na Umaskini, Elimu na Mafunzo ya Wanawake, Afya ya Wanawake, Ukatili dhidi ya Wanawake, Wanawake na Uchumi, Wanawake katika uongozi na maamuzi, Mifumo ya kitaasisi ya maendeleo ya wanawake, Wanawake na Haki za Binadamu, Wanawake na Vyombo vya Habari, Wanawake na Mazingira, Mtoto wa Kike, pamoja na Wanawake katika migogoro ya kivita
Ikumbukwe kuwa mkutano wa Beijing ambao uliandaliwa na Umoja wa Mataifa ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi mbalimbali wanachama wa umoja huo na Tanzania ikiwemo, ambapo iliongozwa na Balozi Getrude Mongella ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo, ambapo inaelezwa kuwa mkutano huo uliweka vipaumbele hivyo ili kuwe na uwajibikaji wa serikali, mashirika ya kiraia na wadau wengine wa maendeleo
Imeelezwa kuwa, hadi kufikia sasa vipaumbele ambavyo vimetekelezwa kwa mafanikio (ingawa kwa kiasi fulani) hapa Tanzania ni Wanawake na Umaskini, Wanawake na Uchumi, Wanawake na Afya, Ukatili dhidi ya Wanawake, Wanawake katika Uongozi na Maamuzi na Mtoto wa kike
“Serikali ya Tanzania katika kutekeleza vipaumbele vya Beijing ilifanya mambo kadhaa ya kusababisha maendeleo kwa kuboresha usawa wa kijinsia nchini, mambo hayo ni pamoja au kurekebisha sheria na taratibu, na hata kufanya maboresho ya Katiba, kwa mfano serikali ya Hayati Rais Benjamin Mkapa ambaye alikuwa madarakani wakati mkutano wa Beijing ulipofanyika, ilifanya mambo makuu manne na serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilifanya jambo moja kubwa ambalo litasherehekewa”, mambo hayo ni kama ifuatavyo:-
(I) Bajeti kwa Taifa kwa mtazamo wa kijinsia: serikali ya Hayati Benjamini Mkapa iliingiza serikalini utaratibu mpya wa kuandaa bajeti ya Taifa kwa mtazamo wa kijinsia (gender budgeting), kuandaa bajeti ya serikali kwa mtazamo wa kijinsia kunawezesha mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijinsia yaliyopo vijijini na mijini, bajeti ya Taifa kuandaliwa kwa mtazamo wa kijinsia kumewezesha wanawake maskini, vijana wa kike na wa kiume na watu wenye ulemavu wanawake na wanaume kupatiwa mikopo ya kuendesha shughuli zao kiuchumi
(II) Sheria ya kudhibiti makosa ya kujamiiana: mwaka 1998 serikali ilipeleka Bungeni Muswada wa sheria ya kudhibiti makosa ya kujamiiana (Sexual Offenses Special Provision Act-SOSPA) na ikapitishwa kuwa sheria, inaelezwa sheria hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika masuala ya ukatili wa kingono, sio tu kwamba jamii zimevunja ukimya kuhusu ukatili huo bali pia juhudi mbalimbali zimefanyika ambapo watu wengi wakiwepo watu mashuhuri mfano mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na watoto wake watatu walipohukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti watoto
(III) Sheria za Ardhi zinazozingatia usawa wa kijinsia: serikali ya Hayati Benjamin Mkapa ilitunga sheria za ardhi zilizotambua usawa wa kijinsia katika kufikia kumiliki na kutoa maamuzi kuhusu raslimali ardhi, mwaka 1999 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimpitisha sheria ya ardhi namba 4 na sheria ya ardhi ya vijiji namba 5, ambapo sheria hizo zilianza kutumika rasmi mwezi Mei mwaka 2001, pia sheria ya Mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi ilipitishwa mwaka 2002 na kuanza kutumika rasmi mwezi Oktoba 2003, moja ya msingi mkuu wa sheria hizo ni kwamba raia wote wa Tanzania wanawake na wanaume wana haki sawa ya kupata, kumiliki, kutumiana kugawa Ardhi
(IV) Kuongeza idadi ya Wanawake kwenye uongozi: mwezi Februari mwaka 2005 serikali ya Hayati Benjamin Mkapa ilifanya mabadiliko ya 14 katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mabadiliko hayo yaliwezesha idadi ya Wabunge wanawake kuwa isiopungua asilimia 30, hivi sasa Bunge la JMT lina jumla ya Wabunge 393 ambapo asilimia 37 ni wanawake lakini wengi wao yaani zaidi ya 100 ni wa viti maalum, harakati za kupigania usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya maamuzi umekuwa ukishikiliwa bango na mashirika mengi ya kiraia hasa TGNP, TAMWA, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Shirika la Wanawake sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF)
(V) Sheria ya mtoto ya mwaka 2009: mafanikio makubwa ya Beijing 30+ ni kutungwa kwa sheria ya mtoto, mwaka 2009 serikali ya Dkt. Jakaya Kikwete ilitunga sheria ya mtoto, ambapo sheria hiyo pamoja na kusaidia, kuimarisha harakati za kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu sawa na mtoto wa kiume kumesaidia pia kuimarisha vuguvugu la kudai mabadiliko ya vifungu vilivyopo kwenye sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambavyo vinaruhusu mtoto wa kike mwenye umri chini ya miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya mzazi au Mahakama.