Maafisa kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakiongozwa na Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho Gilead Teri, Alhamisi Julai 25.2024 wamekutana na wawekezaji wa ndani/wazawa, mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam ambapo lengo la mkutano huo likiwa ni kujadili fursa na changamoto mbalimbali wanazokutananazo katika uwekezaji wao.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo pia umehudhuriwa na maafisa kutoka taasisi mbalimbali wanaofanya kazi sambamba na TIC kwenye kituo cha pamoja (one stop center) ambao ni BRELA, TRA, NIDA nk, sambamba na wawakilishi kutoka Halmashauri za Muheza (mkoani Tanga) na Kisarawe (mkoani Pwani) ambao baadhi yao walitoa mada kwenye mkutano/kongamano hilo
Jambo TV inakuletea mambo makubwa matano (5) yaliyojadiliwa katika mkutano/kongamano la wawekezaji wa ndani/wazawa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kama ifuatavyo:
(i) Mikakati ya kuondoa vikwazo vya Uwekezaji; mkutano huo umejadili mikakati ya kuondoa vikwazo vinavyowakabili wawekezaji wa ndani, ikiwa ni pamoja na mchakato wa utoaji wa leseni na vibali, ili kurahisisha na kufanikisha uwekezaji wa haraka na kwa ufanisi
(ii) Fursa za uwekezaji katika sektabalimbali; washiriki wa mkuyano huo wamepata nafasi ya kujadili fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda, na teknolojia, huku wakisisitiza umuhimu wa kutumia fursa hizo ili kukuza uchumi wa Taifa
(iii) Huduma za TIC kwa wawekezaji; kupitia mkutano huo maelezo yametolewa kuhusu huduma zitolewazo na TIC kwa wawekezaji wa ndani, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kitaalamu na taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kuendeleza miradi yao kwa ufanisi
(iv) Ushirikiano wa serikali na sekta binafsi; mkutano huo umesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kukuza uwekezaji wa ndani, ambapo vongozi wamewahakikishia wawekezaji kwamba serikali itakuwa mshirika wa karibu katika kufanikisha malengo yao ya uwekezaji, na
(v) Matatizo ya kisheria na mipango ya marekebisho; katika mkutano huo imejadiliwa jinsi matatizo ya kisheria yanavyoweza kuathiri uwekezaji wa ndani na mipango ya serikali ya kuboresha mfumo wa sheria na kanuni zinazohusiana na uwekezaji ili kutatua changamoto hizo,
Mkutano huo umeendelea kudhihirisha dhamira iliyowekwa na TIC katika kuhakikisha suala la uwekezaji linakuwa na tija nchini kwa kukutana mara kwa mara na wadau ili kujadili fursa na changamoto zinazojitokeza.