Latest Posts

MANISPAA YA IRINGA YAANZA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA MKUU WA MKOA KUKAMILISHA BWENI SHULE YA SEKONDARI LUGALO

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeanza utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, kwa kupeleka vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Lugalo, mradi uliogharimu shilingi milioni 159.

Ujenzi wa bweni hilo ulikwama kwa muda baada ya wazabuni waliokuwa wakisambaza vifaa vya ujenzi kushindwa kulipwa madeni yao ya nyuma, hali iliyosababisha kusimamishwa kwa shughuli za ujenzi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amechukua hatua za haraka kwa kuhakikisha vifaa vyote muhimu vinafikishwa katika eneo la mradi ili ujenzi huo uendelee na kukamilika kwa wakati. Amesema Manispaa imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wazabuni wote wanaodai madeni yao wanalipwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Kwa upande wake, fundi anayesimamia ujenzi wa bweni hilo, Dickson Mlyuka, ameahidi kukamilisha ujenzi huo ifikapo Februari 15, 2026, akieleza kuwa kwa sasa vifaa vyote muhimu tayari vimepatikana.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Lugalo, Praygod Makongwa, ameishukuru Serikali ya Mkoa na Manispaa ya Iringa kwa kuchukua hatua za haraka, akisema kukamilika kwa bweni hilo kutasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Ikumbukwe kuwa awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akikagua ujenzi wa bweni hilo  alionesha kukerwa na baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo elimu na afya  katika Manispaa ya Iringa kukwama kutokana na wazabuni kutolipwa fedha zao, hatua iliyomsukuma kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi kuhusu madai hayo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!