Latest Posts

MANYERERE: TATIZO LA TANZANIA SI MABEBERU, “BUNDUKI ZILIKUWA ZA WATANZANIA”

Mhariri mwenza wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, amedai chanzo kikuu cha matatizo ya Taifa la Tanzania si mabeberu wala mataifa ya kigeni, bali ni mifumo mibovu na maamuzi ya ndani yanayofanywa na Watanzania wenyewe, akisisitiza kuwa taifa haliwezi kupata suluhu ya kudumu bila kujitazama kwa uaminifu.

Katika makala yake ya Novemba 28, 2025, Manyerere amerejea maonyo ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliyoyatoa miaka 63 iliyopita kwenye kijitabu Tujisahihishe, akieleza kwamba Watanzania wameendeleza tabia ile ile ya kutafuta mchawi nje ya nchi badala ya kukiri makosa ya ndani. Anasema Mwalimu Nyerere alikwishaonya kuwa ni rahisi kulaumu “mabeberu,” “makaburu,” au “watu kutoka nje” kuliko kujikagua na kukubali kuwa “tatizo ni sisi.”

Kwa mujibu wa Manyerere, matatizo mengi yanayoikabili Tanzania kuanzia Katiba iliyojaa mianya, mfumo dhaifu wa uongozi, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, misafara mikubwa ya viongozi, mpaka tume za uchaguzi zisizoaminika hayajaagizwa kutoka nje bali yamejengwa na mifumo na matamanio ya Watanzania wenyewe.

“Beberu gani ameagiza vyombo vya habari viminywe? Ni uamuzi wa viongozi wetu na mfumo tulioujenga kwa mikono yetu wenyewe. Sasa baada ya udini kukwama, tunahamasishwa tuamini kuwa madhila yetu yanasababishwa na mabeberu! Kama yapo, ni kidogo sana. Mengi ni matokeo ya kazi ya akili, matamanio na ubinafsi wa watawala wetu”, ameeleza.

Aidha, Manyerere anataja ubaguzi wa kielimu unaowatenga watoto wa wananchi wa kawaida, matumizi makubwa ya posho na misafara ya kifahari, pamoja na barabara kufungwa ili viongozi wapite, akisema hakuna hata moja lililoelekezwa na mkoloni au taifa lolote la kigeni. Ameongeza kuwa vitendo vya rushwa, mikataba mibovu, maamuzi yasiyoangalia maslahi ya taifa, pamoja na ukosefu wa uthubutu wa kuwajibishana ni matokeo ya mifumo dhaifu iliyojengwa na Watanzania wenyewe.

“Kwa miaka mingi, rushwa imeota mizizi kuanzia juu hadi chini. Hakuna mkoloni aliyeagiza tuibe asilimia 10 kwenye miradi ya serikali, tuidhinishe mikataba mibovu, au tuoneane aibu tunapopaswa kuwajibishana. Huu ni udhaifu wa ndani, si njama za nje. Aidha, mauaji, utesaji, watu kutekwa na kutopotea, yamekuwa majeraha ya taifa letu bila kushinikizwa na taifa lolote kubwa”, ameandika Manyerere.

Akirejea maafa ya Oktoba 29, Manyerere anasema yaliyotokea hayakupangwa na mabeberu, kwani “bunduki zilishikwa na Watanzania, maamuzi yalifanywa na taasisi zetu, na mipango ilitoka ndani ya mfumo wetu wenyewe.” Anaonya kuwa kutafuta mchawi nje ya Tanzania ni kukwepa ukweli muhimu unaoweza kuokoa taifa.

Akinukuu tena maneno ya Mwalimu Nyerere katika Tujisahihishe, Manyerere anasisitiza kwamba majibu ya haraka na ya kukwepa ukweli ndiyo yanayolizuia taifa kutafuta suluhu za kweli. Anasema ukombozi wa Tanzania upo mikononi mwa Watanzania wenyewe kwa kujenga mifumo mipya, kuondoa tabia mbovu, kubadili uongozi na kuandika Katiba Mpya.

Manyerere ameongeza kuwa urithi mkubwa ambao Rais Samia Suluhu Hassan anaweza kuuacha ni “kufumua na kujenga upya mifumo mibovu inayoliangamiza taifa,” akisisitiza kuwa bado ana nafasi ya kufanya hivyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!