Mbunge wa jimbo la Manyoni Mashariki Mkoani Singida Mhe. Dkt. Pius Chaya aimepongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia hapa nchini.
Akizungumza leo Septemba 13, 2024 katika ofisi za TEA Jijini Dodoma Dkt. Chaya amesema, ameshuhudia miradi mingi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, mabweni, nyumba za walimu pamoja na maktaba za Sayansi ambazo zimejengwa na TEA.
Dkt. Chaya ammtembelea Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha ofisini kwake kwa lengo la kutoa shukrani kwa miradi ya elimu jimboni kwake ambayo amesema imesaidia katika kuinua ubora wa elimu.
“Jimboni kwangu Manyoni Mashariki ni wanufaika wa miradi inayotekelezwa na TEA hivyo nimekuja pamoja na diwani kuwashukuru sana kwa miradi hiyo, amesema Dkt. Chaya.”
Ameitaja miradi ya elimu ambayo imefadhiliwa na TEA jimboni Manyoni Mashariki kuwa ni ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Sasajila, vyumba vitatu vya madarasa shule ya msingi Sanza na Kintinku pamoja na matundu 24 ya vyoo shule ya msingi Kintinku.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha amemshukuru Mbunge huyo kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi hiyo hadi imekamilika.