Mamlaka mpya inayoongozwa na waasi nchini Syria imeripoti kuwa maafisa 14 wa wizara ya mambo ya ndani wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na vikosi vinavyomtii Rais aliyepinduliwa Bashar al-Assad. Tukio hilo lilitokea Jumanne karibu na bandari ya Mediterranean ya Tartous.
Ripoti za awali zinaeleza kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikijaribu kumkamata afisa wa zamani aliyekuwa akihusishwa na vitendo katika gereza maarufu la Saydnaya, karibu na mji mkuu Damascus, wakati waliposhambuliwa. Shirika la Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR), lenye makao yake Uingereza, liliripoti kuwa wanamgambo watatu wa kundi la waasi pia waliuawa katika mapigano hayo. Vikosi vya usalama baadaye vilifanikiwa kurejesha udhibiti wa eneo hilo.
Machafuko yameendelea kuikumba Syria baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Bashar al-Assad zaidi ya wiki mbili zilizopita, kufuatia mapinduzi yaliyoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).
Hali ya wasiwasi pia imetanda katika mji wa kati wa Homs, ambako mamlaka ziliweka amri ya kutotoka nje usiku kucha baada ya machafuko yaliyotokea kufuatia kusambaa kwa video inayodaiwa kuonesha shambulio dhidi ya hekalu la Alawite.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria ilisema video hiyo ni ya zamani, kutoka kwenye mashambulizi ya waasi huko Aleppo mwishoni mwa Novemba, na ikadai kuwa machafuko hayo yalichochewa na makundi yasiyojulikana.
SOHR iliripoti kuwa mtu mmoja aliuawa na watano kujeruhiwa katika maandamano hayo, ambayo pia yalienea katika miji ya Tartous, Latakia, na Qardaha, mji wa kuzaliwa kwa Bashar al-Assad.
Machafuko haya yameonesha ukosefu wa utulivu nchini Syria, hasa kutokana na mgawanyiko wa kidini na kikabila. Familia ya Assad inatoka katika dhehebu la Alawite, kundi la wachache ambalo lilidhibiti utawala wa Syria kwa zaidi ya miaka 50.
Mashambulizi makali ya HTS, yaliyotokea kaskazini-mashariki mwa Syria na kuenea nchi nzima, yalisababisha kumalizika kwa utawala wa Assad. Pamoja na kuondolewa kwake, changamoto za kuhakikisha usalama na mshikamano wa kitaifa zinaonekana kuwa kubwa, huku maandamano na mashambulizi ya mara kwa mara yakiongeza hali ya taharuki.