Daktari bingwa wa Hospitali ya Kairuki, Dk. Fredy Rutachunzibwa ambaye ni Mtanzania wa kwanza kufuzu mafunzo ya kutibu saratani kwa kutumia teknolojia ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), ameeleza namna tiba hiyo inavyotolewa bila upasuaji.
Akizungumza Novemba 24, 2024, Dk. Rutachunzibwa amefafanua kuwa HIFU inapunguza maumivu, hatari ya maambukizi, na muda wa kupona kwa wagonjwa wa saratani, na kwa kuwa teknolojia hiyo ni ya kisasa zaidi, hutumia mawimbi ya sauti yenye nguvu kuharibu seli za saratani kwa usahihi bila kuhitaji upasuaji wa aina yoyote.
Amesema teknolojia hiyo inatoa suluhisho kwa wagonjwa wengi wa saratani, hasa wale wanaokosa matibabu ya kisasa kutokana na vikwazo vya kifedha au umbali wa hospitali, na kwamba matibabu kwa kutumia HIFU hayaingizi chochote ndani ya mwili.
“Ngozi haiguswi na hakuna kidonda kinachotengenezwa, hakuna nusu kaputi, yaani mgonjwa anaondolewa uvimbe huku akiwasiliana na daktari anayemhudumia,” amesema na kuongeza,
“Kinachofanyika ni kwamba mawimbi sauti yanapelekwa katika eneo lenye uvimbe unaunguzwa bila kuathiri sehemu zingine na matibabu haya yanatolewa kwa wenye saratani za aina mbalimbali”.
Dk. Rutachunzibwa, aliyefuzu mafunzo haya nchini China mwaka 2023, amesema teknolojia ya HIFU ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya nchini Tanzania, kwani inaboresha huduma za afya kwa kuongeza ufikiaji wa matibabu ya kisasa na kupunguza vifo vinavyosababishwa na saratani nchini Tanzania.
“Awali, wagonjwa walilazimika kusafiri kwenda mataifa yaliyoendelea kupata matibabu haya, lakini sasa huduma hii inapatikana hapa nchini katika Hospitali ya Kairuki,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Dk. Rutachunzibwa, Hospitali ya Kairuki ni ya kwanza nchini Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kutumia teknolojia ya HIFU, na ni ya tatu Barani Afrika.