Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, na wafanyakazi wengine wa Umoja wa Mataifa wamenusurika shambulio la anga lililofanywa na Israel katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa, Yemen, siku ya Alhamisi.
Kupitia chapisho lake katika mtandao wa kijamii, Tedros amesema kuwa walikuwa karibu kupanda ndege wakati shambulio hilo lilipotokea. “Mmoja wa wafanyakazi wa ndege yetu alijeruhiwa,” aliandika, huku akibainisha kuwa watu wawili waliokuwepo uwanjani waliuawa.
Mashambulizi hayo, ambayo pia yalilenga vituo vya umeme na bandari, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua watatu na kujeruhi zaidi ya dazeni moja, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vinavyoendeshwa na waasi wa Houthi.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilithibitisha kuhusika katika mashambulizi hayo, likisema kuwa ndege zake za kivita zilifanya mashambulizi ya kijasusi kwenye shabaha za kijeshi za Houthi katika maeneo ya pwani ya magharibi na ndani ya Yemen. IDF ilieleza kuwa ililenga “miundombinu ya kijeshi” katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa, vituo vya umeme vya Hezyaz na Ras Kanatib, pamoja na maeneo katika bandari za Al-Hudaydah, Salif, na Ras Kanatib.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amdsema kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi za “kukata mkono wa kigaidi wa mhimili wa uovu wa Iran.” Alisisitiza kuwa “tunaanza tu na Wahouthi.”
Mohammed Ali al-Houthi, mkuu wa kamati kuu ya mapinduzi ya Houthis, amelaani mashambulizi hayo akiyaita “ya kinyama” na “uchokozi.” Kundi hilo la waasi, linaloungwa mkono na Iran, limepinga vikali hatua hizo za Israel, likisema kuwa ni dhihirisho la kupuuzia maisha ya raia na sheria za kimataifa.
Mashambulizi haya yanakuja katika wakati ambapo Yemen bado inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu uliosababishwa na vita vya muda mrefu kati ya vikundi vya waasi na serikali inayotambuliwa kimataifa. Taarifa za awali hazijathibitisha iwapo waliouawa ni raia wa kawaida au wapiganaji wa Houthi.