Latest Posts

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SERIKALI

Imeelezwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 79 zilitumika kufanikisha miradi mbalimbali ya elimu nchini Tanzania kwa mwaka 2023, kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

Akizungumza katika kikao kazi kati ya Wizara na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) mkoani Dar es Salaam, Desemba 13, 2024, Waziri Gwajima amebainisha kuwa fedha hizo zilitumika katika miradi na afua zinazolenga kuboresha elimu na ustawi wa jamii.

“Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023, sekta ya elimu ilitumia shilingi 79,166,785,015 kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule, utoaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, na kuwajengea uwezo walimu. Huu ni ushahidi wa mchango mkubwa wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya taifa,” amesema Waziri Gwajima.

Waziri Gwajima amefafanua kuwa miradi iliyotekelezwa ni pamoja na programu za kuzuia ukatili wa kijinsia na kwa watoto, ujasiriamali, mafunzo ya kompyuta, elimu ya usalama barabarani, na kuwezesha watoto wa kike kubaki shuleni. Aidha, mashirika hayo yamekuwa yakitoa ufadhili wa masomo, samani za shule, na sare kwa wanafunzi.

“Mashirika yamefanya kazi kubwa kusaidia jamii, lakini lazima tuhakikishe kwamba miradi hii inatekelezwa kwa uwiano mzuri ili maeneo yote ya nchi yanufaike.” Amesema Gwajima.

Katika kikao kazi hicho, washiriki wametakiwa kujadili changamoto zinazokumba mashirika yasiyo ya kiserikali katika sekta ya elimu. Waziri Gwajima amesisitiza kuwa ushirikiano wa sekta mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango bora.

“Lazima tushirikiane, siyo tu kati ya serikali na mashirika, bali pia ndani ya mashirika yenyewe ili kuepuka miradi inayorudia maeneo au yenye kasoro za utekelezaji,” ameeleza.

Akirejea kikao kazi cha awali kilichofanyika Novemba 24, 2024, jijini Arusha, Waziri Gwajima alisema kuwa jumla ya maazimio 12 yalipitishwa na mengi tayari yameanza kutekelezwa.

“Ni matumaini yangu kuwa majadiliano ya leo yatazalisha mapendekezo yanayotekelezeka, na kwa pamoja, tutaimarisha mchango wa mashirika haya katika maendeleo ya taifa,” amehitimisha Waziri.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!