Latest Posts

MASWALI YASIYOPATA MAJIBU MAUAJI YA MTOTO GRAYSON

Na; mwandishi wetu, Dodoma.

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita (6) Grayson Kanyenye hivi karibuni ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na watu wasiojulikana jijini Dodoma

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi amethibitisha kuuawa kwa mtoto huyo na kueleza kuwa tukio hilo limegundulika asubuhi ya tarehe 25 Desemba, 2024 maeneo ya nyumbani kwao Ilazo Extension, jijini humo baada ya mama wa mtoto huyo kurudi kutokea matembezini na kukuta mtoto wake ameuawa

Kamanda Katabazi amesema wakati mtoto huyo anauawa mama yake hakuwepo nyumbani alikuwa ameenda matembezi na ndipo aliporudi alimkuta mtoto wake ameshafariki, hata hivyo mpaka sasa Jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja anayejulikana kwa jina la kelvin Gilbert ambaye ni dereva bodaboda ambaye ndiye aliyeachiwa mtoto huyo na mama yake, huku likiendelea kumtafuta mtuhumiwa mwingine, na uchunguzi juu ya kuuawa kwa mtoto huyo ukiwa unaendelea

Sasa pamoja na yote bado kuna maswali lukuki yanayoibuka juu ya kifo cha mtoto huyo, na kile kilichojificha nyuma ya pazia

Maswali yasiyokuwa na majibu; kifo cha Grayson kimeacha maswali mengi ambayo bado hayajapata majibu, miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na je, ni nani hasa aliyefanikisha ukatili huu?, na ni nini kilichosababisha tukio hili?, je mauaji haya yalipangwa, au ni ajali ya kijinai?, haya yote ni maswali na mengine mengi yanayoibuka lakini ukweli unabaki kwamba maswali hayo hayana majibu

Kwa sasa, wakazi wa Dodoma na pengine Watanzania kwa ujumla wake wanasubiri kwa shauku kubwa matokeo ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi, huku wakiwa na maombi ya haki kutendeka kwa mtoto huyo asiye na hatia

Kwingineko kama inavyofahamika, familia ya Grayson imekumbwa na majonzi, vilio na simanzi huku jamii nzima ikiwa na kwenye dimbwi la hofu na mtanziko mkubwa  juu ya usalama wa watoto wao ndani na nje ya mazingira yanayowazunguka

Kifo cha mtoto Grayson si tu kimeleta simanzi, bali pia kimeibua hitaji la dharura la kuimarisha ulinzi wa watoto na kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya ukatili, ni matumaini ya wengi kwamba uchunguzi huo unaoendeleshwa na Jeshi la Polisi utaleta ukweli na kuhakikisha haki inatendeka kwa familia ya marehemu

Jambo TV kama taasisi huru ya kihabari tutazidi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hili na kuwaletea taarifa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea, na pale zinapotufikia

Hata hivyo, hadi sasa watu wanaenda mbali na kuhusishaa tukio hili na imani za kishirikina huku wengine wakishangazwa na kuzikwa kwa haraka mtoto huyo kabla ya uchunguzi wa Polisi kukamilika, ambapo kwa mjibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi amenukuliwa akisema mara kadhaa kwamba, “chunguzi unaendelea”

Aidha, kifo cha mtoto Grayson Kanyenye, mwenye umri wa miaka sita (6) kimeendelea kuzua mjadala mzito miongoni mwa wakazi wa Dodoma na viunga vyake, huku baadhi ya watu wakihusisha tukio hilo na imani za kishirikina, uhuma hizo zimepata nguvu kutokana na giza lililotanda juu ya kifo cha mtoto huyo na namna maelezo yanavyokinzana miongoni mwa wadau

Kwa mujibu wa maoni ya baadhi ya wananchi wanaeleza kuwa, tukio hilo linaweza kuwa limechangiwa na kafara zinazohusiana na imani za kishirikina, hali ambayo imezidi kuzua taharuki, haraka ya kumzika marehemu, pamoja na mazingira ya kifo chake, vimewaacha wengi wakijiuliza maswali mengi bila majibu

Jeshi la Polisi latoa onyo dhidi ya tetesi; kwakuwa hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa tukio hili lina uhusiano na masuala ya kishirikina au kafara, ni vyema wananchi watulie na kuruhusu vyombo vya sheria kufanya kazi yake

Jamii imekumbwa na hofu kubwa, hasa kutokana na kuongezeka kwa tetesi hizo, wakazi na waombolezaji waliojitokeza msibani wameitaka serikali kuchukua hatua stahiki na madhubuti kuhakikisha usalama wa watoto unaimarishwa

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa kidini wamejitokeza kupinga matukio ya kikatili wakisisitiza kuwa ni muhimu jamii kuwa na roho ya ubinadamu na kumrudia Mwenyezi Mungu

Matarajio ya jamii kwa sasa, wananchi wanatarajia uchunguzi wa kina ambao utatoa mwanga kuhusu chanzo halisi cha tukio hilo, wengi wanasubiri kwa hamu kuona kama mtuhumiwa aliyekamatwa na Polisi, Kelvin Gilbert, ataunganishwa na tukio hilo au kama Polisi watagundua wahusika wengine nyuma ya pazia

Katika kipindi hiki cha simanzi, wito kwa jamii unaotolewa ni kuendelea kushikamana na kutoa msaada kwa familia ya marehemu huku wakiheshimu mchakato wa uchunguzi, kifo cha mtoto Grayson kinapaswa kuwa somo la kuimarisha mshikamano wa jamii dhidi ya vitendo vya kikatili na kuhakikisha usalama wa watoto wote unapewa kipaumbele.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!