Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea katika msimu wa 2021/2022, Sekta ya Kilimo ilikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la ndani kutokana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia.
Imesema bei za mbolea nchini zilipanda kutoka wastani wa shilingi 70,000/= kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufika shilingi 140,000/= hadi 150,000/= kwa mfuko, hali hoyo ilichangia kushuka kwa matumizi ya mbolea, tija na uzalishaji.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Jumatatu Machi 19, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema “Mpango huu maalumu wa ruzuku ya mbolea uliwezesha kupunguza gharama ya mbolea na kufanya wakulima kununua mbolea kwa bei ya shilingi 40,000/= hadi 80,000/= kwa kutegemea aina ya mbolea na umbali sawa na punguzo la takribani asilimia 50 ya bei”
kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Serikali inatekeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea kwa kutoa ruzuku kwa wakulima wote na kwa mazao yote nchini”
Aidha amesema kuwa tofauti na ruzuku zilizopita, katika awamu hii ruzuku ya mbolea inatolewa kupitia Mfumo wa Kidijitali wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System) ambao unatumika kusajili wakulima, waingizaji, wazalishaji na mawakala wa mbolea pamoja na kuratibu usambazaji na mauzo.
Aidha Matumizi ya mfumo wa kidijitali katika kusambaza mbolea ya ruzuku umeinufaisha Serikali hususani katika kuwezesha kuanzisha kanzidata ya kuaminika ya wakulima, Mawakala wa mbolea, Waingizaji na Wazalishaji wa mbolea Nchini.
“mfumo huu wa kidijitali umekuwa nyenzo muhimu ya ufuatiliaji na uendeshaji wa biashara ya mbolea nchini kuanzia mbolea inavyoingizwa au kuzalishwa kwenye viwanda vya ndani hadi inapouzwa kwa mkulima katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mfumo huu umerahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za matumizi ya mbolea nchini pamoja na kudhibiti udanganyifu katika mpango wa ruzuku ya mbolea”
Mbali na hayo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mamlaka imeanzisha Maabara ya kisasa ya mbolea ambapo Tanzania inakuwa Nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Maabara mahususi ya mbolea,maabara hii inauwezo wa kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea,hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha udhibiti wa ubora wa mbolea nchini.
Hata hivyo maabara hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania, kama vile Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, na Rwanda.
Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, biashara ya mbolea nchini imekua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.
Pia, matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024, huku lengo likiwa kufikia tani milioni moja ifikapo 2030.