Latest Posts

MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YAPUNGUZA VITENDO VYA RUSHWA MAHAKAMANI

Matumizi ya teknolojia katika usikilizwaji wa mashauri kwenye mahakama nchini Tanzania yametajwa kupunguza malalamiko ya vitendo vya rushwa na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa wakati.

Dkt. Angelo Rumisha, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Morogoro.

Amesema kuwa kabla ya kuanza kutumia teknolojia, kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto za upatikanaji wa haki.

“Kabla ya matumizi ya teknolojia, kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu ucheleweshaji wa haki. Sasa hivi, matumizi ya teknolojia yamepunguza malalamiko hayo na kurahisisha ufanyaji kazi kwa mahakimu na majaji, pamoja na kuondoa changamoto ya kuahirishwa kwa mashauri mara kwa mara,” alisema Dkt. Rumisha.

Aliongeza kuwa mfumo wa kusajili mashauri mtandaoni umeleta ufanisi mkubwa katika utoaji haki.

“Sasa hivi, kesi zote zinasajiliwa mtandaoni, mlalamikaji anaweza kusajili hata saa nane usiku mtandaoni na kupata maelekezo ya moja kwa moja, na kesi yake inapangiwa hakimu au jaji bila kupitia kwa karani,” alifafanua.

 

Dkt. Rumisha pia amesisitiza umuhimu wa jamii kuelewa na kushiriki katika mchakato wa utoaji haki, hasa katika suala la ushahidi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa mkoani Morogoro wamesema kuwa sasa wana imani zaidi na mahakama kutokana na uwazi ulioongezeka, ikiwa ni pamoja na utoaji wa nakala za hukumu kwa lugha ya Kiswahili.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!