Latest Posts

MAUAJI YA MZEE KIBAO YAFUNIKA TAIFA KWENYE WIMBI LA HUZUNI NA WASIWASI, SHINIKIZO LA UWAJIBIKAJI LAONGEZEKA

Tarehe 9 Septemba, 2024 Mzee Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa Sekretarieti Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), atapumzishwa katika makazi yake ya milele baada ya tukio la kikatili lililoacha maswali mengi miongoni mwa Watanzania.

Mauaji yake yamezua hofu, wasiwasi, na hasira, huku watu wengi wakiitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika.

Katika tamko lililotolewa tarehe 8 Septemba, 2024 kupitia mitandao yake ya kijamii, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa maagizo kwa vyombo husika vya uchunguzi kutoa taarifa ya kina kuhusu mauaji hayo.

“Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii.”, aliandika Rais Samia.

Ujumbe huo umewasha hisia mpya ya kutaka uwajibikaji zaidi miongoni mwa viongozi waandamizi wanaosimamia vyombo vya usalama, hata hivyo, wengi wa watumiaji wa mitandao ya kijamii wameeleza kutoridhishwa na kauli hiyo, wakisema haitoshi ikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura, na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jesi la Polisi, Awadh Juma bado wapo madarakani licha ya ongezeko la matukio ya utekaji na mauaji ya raia nchini.

“Wote wajiuzulu kutokana na wimbi la utekaji na mauaji ya raia nchini,” ulisomeka ujumbe mmoja wa mtumiaji wa mitandao ya kijamii.

Ismail Jussa, mwanachama wa ACT Wazalendo, ameongeza shinikizo kwa kusema, “Uchunguzi huru wa kimahakama tu, tena uwe huru, ndio unaweza kutupa ukweli kuhusu matukio haya ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini. Na wakati tunasubiri hatua hiyo, hawa wawili (Masauni na Wambura) wanapaswa kuondolewa bila kuchelewa kwa kushindwa kazi!”

Naye Martin Masese, pia kupitia X, amesema, “Kama kweli Rais Samia ameumizwa na kukerwa na tukio la Mzee Kibao kutekwa, kuteswa, na kuuawa, tungeona hadi sasa kuna watu wamewajibishwa, akiwemo Masauni. Huwezi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati watu wanatekwa na kuuawa.”

Hofu ya usalama imeongezeka huku wananchi wengi wakielezea haja ya kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi ili kulinda usalama wa raia. Mbali na shinikizo kwa Serikali, watu mbalimbali wameeleza huzuni yao kwa familia ya marehemu Mzee Kibao, huku wengi wakisisitiza kuwa haki lazima itendeke.

Mzee Kibao anapumzishwa, lakini hisia kali za wananchi zinaendelea kufukuta, zikitaka majibu ya nani waliohusika na tukio hili na lini watachukuliwa hatua za kisheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!