Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mstaafu Mbarouk S. Mbarouk, amewataka mawakala wa vyama vya siasa kutoingilia kazi ya waandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika vituo vya uandikishaji.
Jaji Mbarouk ametoa kauli hiyo jijini Kibaha, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uboreshaji wa Daftari hilo kwa watendaji wa tume kutoka halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani.
“Mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo vituoni, lakini hawapaswi kuingilia utendaji kazi wa waandikishaji. Hii itasaidia kuweka uwazi na kuepusha vurugu zisizokuwa na lazima,” amesema Jaji Mbarouk.
Ameongeza kuwa Tume imetoa vibali kwa asasi za kiraia 157 kutoa elimu ya mpiga kura na asasi 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo, huku akihimiza ushirikiano kwa taasisi hizo zitakapofika kwenye maeneo husika.
Kwa upande wake, Afisa Uandikishaji wa Wilaya ya Mkuranga, Waziri Kombo, amesema wilaya hiyo imeandaa vituo 578 vya uboreshaji wa Daftari ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kujiandikisha kwa urahisi.
Naye Afisa Uandikishaji wa Wilaya ya Kibaha, Adinani Livamba, amesema zoezi hilo linawahusu wale waliotimiza umri wa miaka 18, pamoja na waliobadilisha makazi yao na wanaohitaji kusahihisha taarifa zao.
Kwa upande wake, Afisa Uandikishaji wa Halmashauri ya Chalinze, Archanus Kilaji, amesema mitambo mpya ya uboreshaji wa Daftari imeboreshwa na mafunzo hayo yatawasaidia watendaji kuimudu kikamilifu.